HomeHabariWaterAid yakabidhi mradi wa WASH milioni 648/- Hanang

WaterAid yakabidhi mradi wa WASH milioni 648/- Hanang

HANANG’, MANYARA — Shirika la WaterAid limekabidhi mradi wa maji na usafi wa mazingira (WASH) wenye thamani ya Shilingi milioni 648.8 katika Kijiji cha Gidamula wilayani Hanang’, mkoani Manyara, ukiwa na lengo la kuboresha maisha ya zaidi ya wakazi 2,440 wa eneo hilo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi na makabidhiano ya mradi huo katika Shule ya Msingi Kidamula, Mkurugenzi wa WaterAid Tanzania, Anna Mzinga, amesema mradi huo una vipengele tisa vinavyolenga kuboresha huduma za maji, usafi na afya ya jamii kwa muda mrefu.

Amesema miongoni mwa vipengele vilivyotekelezwa ni ujenzi wa vyumba maalumu vya kubadilishia taulo za kike na maeneo salama ya kutupia taka za hedhi, hatua inayolenga kuongeza heshima, usiri na usafi kwa wanafunzi wa kike.

“Vifaa hivi si tu miundombinu ya matofali na saruji, bali ni ishara ya heshima na utu kwa wasichana shuleni. Uwekezaji huu unalenga kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya kujifunza katika mazingira salama na yenye heshima,” amesema Mzinga.

Amefafanua kuwa mradi huo umejumuisha mfumo wa maji unaostahimili mabadiliko ya tabianchi, wenye tanki la chini ya ardhi, pampu za nishati ya jua pamoja na miundombinu ya kuvuna maji ya mvua, ambayo imebuniwa kudumu kwa angalau miaka 15.

Aidha, mradi umehusisha ujenzi wa vyoo 17 vinavyozingatia jinsia na ujumuishi kwa wanafunzi na walimu, pamoja na kuwekwa kwa vifaa vya kunawa mikono ili kudhibiti maambukizi ya magonjwa shuleni.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Semidu, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amelipongeza shirika la WaterAid kwa mchango wake katika kusaidia serikali kuboresha huduma za maji, afya na usafi wa mazingira.

Amesema serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, huku akisisitiza umuhimu wa kutunza miundombinu hiyo ili idumu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Wananchi wa Kijiji cha Gidamula wameeleza kufurahishwa na mradi huo, wakisema kwa muda mrefu walikuwa wakikabiliwa na uhaba wa maji na kulazimika kutembea umbali mrefu kuyatafuta, hali iliyokuwa ikiathiri maisha yao ya kila siku.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments