DAR ES SALAAM — Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amepokea Taarifa ya Sensa ya Wanyamapori ya Taifa ya Mwaka 2024/2025 iliyowasilishwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) Ikulu, Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais Samia ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na TAWIRI kwa kufanikisha zoezi hilo kubwa la kitaifa ambalo kwa mara ya kwanza limefadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali.
Rais Samia amesema matokeo ya sensa hiyo yanaonesha mafanikio makubwa ya juhudi za uhifadhi nchini na kuthibitisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa mataifa yenye utajiri mkubwa wa wanyamapori duniani.


Aidha, ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa rasilimali za asili ili Watanzania waone thamani ya urithi huo na kushiriki kikamilifu katika kuutunza kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuwajengea watoto na vijana uelewa wa wanyamapori wa Tanzania kwa kuwafundisha majina yao ya Kiswahili na kuimarisha utamaduni wa kuthamini urithi wa taifa tangu wakiwa wadogo.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amemshukuru Rais Samia kwa kuwezesha utekelezaji wa sensa hiyo kwa kutenga fedha za ndani, hatua iliyowezesha Tanzania kufanya sensa ya kitaifa ya wanyamapori kwa kutumia rasilimali zake.
Amesema sensa hiyo inayofanyika kila baada ya miaka 10 inalenga kubaini idadi, mtawanyiko, mwenendo na hali ya ustawi wa wanyamapori pamoja na changamoto zinazoathiri mifumo ya ikolojia na sekta ya utalii.
Matokeo ya sensa iliyofanyika kati ya Septemba 2024 na Oktoba 2025 yanaonesha uwepo wa spishi 28 za wanyamapori wa kati na wakubwa katika mifumo mbalimbali ya ikolojia nchini, huku yakionesha mwenendo chanya wa uhifadhi katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Aidha, matokeo ya kina ya sensa hiyo yanatarajiwa kutangazwa rasmi na Wizara ya Maliasili na Utalii.





