Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania imejipanga kuwa moja ya vituo vikuu vya uwekezaji barani Afrika kwa kufungua milango kwa kampuni za kimataifa kuwekeza katika miradi mikubwa ya kimkakati.
Dkt Samia amesema miongoni mwa maeneo yanayohitaji ushirikiano wa wawekezaji ni pamoja na maendeleo ya bandari, maeneo maalumu ya kiuchumi na sekta za uzalishaji zitakazochochea ukuaji wa uchumi na ajira kwa Watanzania.
Akizungumzia mradi wa kimkakati wa Bagamoyo, Rais Dkt Samia amesema :“Mradi wa Eneo Maalumu la Kiuchumi la Bagamoyo (BSEZ) ni mradi namba moja ambao tunakaribisha kampuni za kimataifa kushirikiana nasi.”
Dkt Samia ameeleza hayo leo Juni 5,2026 katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF) 2026, nchini Urusi katika mwendelezo wa ziara yake ya kikazi katika Taifa hilo. Katika mkutano uliuhudhuriwa na Rais wa Urusi, Vladmir Putin.
Kauli hiyo ya Dkt Samia inaonyesha namna Tanzania ilivyojijengea taswira mpya duniani kama nchi yenye mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji, huku Serikali ikiendelea kuweka miundombinu na sera zinazovutia mitaji ya ndani na nje ya nchi.




