HomeHabariDC Ilala atangaza vita dhidi ya madanguro

DC Ilala atangaza vita dhidi ya madanguro

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ametangaza msako mkali dhidi ya madanguro na vitendo vya ukiukwaji wa maadili, akisisitiza kuwa Serikali haitamvumilia mtu yeyote anayehusika na biashara hizo au kuwatumia watoto katika vitendo vya unyanyasaji.

Akizungumza na wananchi jijini Dar es Salaam, Mpogolo alisema Serikali imejipanga kuhakikisha inatokomeza vitendo vinavyohatarisha usalama na maadili ya jamii, huku akilipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua za haraka za kuwakamata watuhumiwa.

Alisema taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa katika Kata ya Zingiziwa kulikuwa na mtu anayeshukiwa kuwatumia watoto wa kike kuwachezesha wakiwa uchi kwa malipo ya kati ya Shilingi 3,000 na 5,000, akieleza kuwa kitendo hicho ni ukatili mkubwa na ukiukwaji wa maadili.

Kwa mujibu wa Mpogolo, mtuhumiwa huyo tayari amekamatwa na Jeshi la Polisi na uchunguzi unaendelea. Amewataka wananchi kutomkingia kifua mtu yeyote anayekabiliwa na tuhuma hizo na kuziacha mamlaka husika zitekeleze wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

“Niwapongeze sana Jeshi la Polisi kwa umakini wao. Wamechukua hatua mapema kabla madhara hayajaongezeka. Ushahidi uliopo utawezesha sheria kuchukua mkondo wake,” amesema.

Aidha, amewataka wenyeviti wa mitaa, viongozi wa dini na wananchi kushirikiana na vyombo vya dola katika kutokomeza madanguro na vitendo vinavyoharibu maadili, akisisitiza kuwa umaskini hauwezi kuwa sababu ya kuwahusisha watoto au wanawake katika vitendo vinavyodhalilisha utu wa binadamu.

Mpogolo pia ameipongeza Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) pamoja na Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) kwa operesheni zilizofanyika hivi karibuni, akibainisha kuwa zaidi ya watu 20 wamekamatwa katika msako dhidi ya vitendo hivyo.

Amesema operesheni hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kulinda watoto, kurejesha maadili na kuimarisha usalama wa wananchi katika Wilaya ya Ilala.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments