Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umepokea gawio la Sh bilioni 1.07 kutoka mradi wa Rock City Mall jijini Mwanza, ikiwa ni sehemu ya jumla ya Sh bilioni 1.18 zilizogawiwa kwa wabia watatu wa mradi huo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, amesema gawio hilo linaonesha umuhimu wa kusimamia uwekezaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii ili kulinda michango ya wanachama na kuizalishia faida.
Akizungumza jijini Dodoma, Oktoba 27, 2026, wakati wa hafla ya kukabidhi gawio hilo, Sangu amesema uwekezaji wenye tija unaweza kuchangia ukuaji wa uchumi na uzalishaji wa ajira nchini.
Katika mgawo huo, Halmashauri ya Jiji la Mwanza imepokea Sh milioni 71.3, huku Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ikipokea Sh milioni 47.56. PSSSF ndiyo mwekezaji mkuu katika mradi huo kupitia Kampuni ya Mwanza Rock City Ltd.




“Ninapenda kutoa pongezi kwa Bodi na Menejimenti ya mifuko yetu ya hifadhi ya jamii, hususan PSSSF, kwa kuhakikisha michango ya wanachama inalindwa, inakua na kurejesha faida kwa Taifa,” amesema Sangu.
Amesema mradi huo una mchango katika maendeleo ya Mwanza na ajira, akibainisha kuwa asilimia 98 ya jengo hilo lina wapangaji na zaidi ya watu 1,000 wananufaika na ajira za kudumu na za muda zinazohusiana na shughuli za mradi.
Sangu ameitaka PSSSF na taasisi nyingine zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kufuata miongozo ya uwekezaji ya Benki Kuu ya Tanzania pamoja na sera za uwekezaji za taasisi husika ili kuhakikisha fedha za wanachama zinawekezwa kwa tija.
Amesema lengo la uwekezaji huo ni kulinda thamani ya michango ya wanachama na kusaidia kuhakikisha wanapata mafao wanapostaafu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Fortunatus Magambo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mwanza Rock City Company Limited, amesema gawio hilo ni matokeo ya uwekezaji ulioanza kuzaa matunda.
Magambo amesema Rock City Mall inarahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa kuwakutanisha wafanyabiashara, benki, migahawa na watoa huduma wengine katika eneo moja, huku ikitoa fursa za biashara na ajira.
Ameeleza kuwa uwekezaji wa PSSSF unazingatia mwongozo wa Benki Kuu ya Tanzania na sera ya mfuko huo. Sehemu kubwa ya uwekezaji wake ipo katika dhamana za Serikali, hisa za kampuni na amana za benki, huku majengo yakiwa sehemu mojawapo tu ya uwekezaji huo.









