HomeHabariSerikali yaipa TPDC vitalu vinne vya utafutaji mafuta, gesi

Serikali yaipa TPDC vitalu vinne vya utafutaji mafuta, gesi

Serikali imesisitiza umuhimu wa kuhakikisha Watanzania, hususan vijana na kampuni za ndani, wanapata manufaa ya moja kwa moja kutokana na shughuli za utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia, ikiwemo ajira, mafunzo, teknolojia na zabuni.

Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, amesema hayo Oktoba 28, 2026, katika hafla ya utiaji saini leseni za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika vitalu vya Mnazi Bay North, West Songo Songo, Eyasi Wembere na Lindi-Mtwara, iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Ndejembi amesema utekelezaji wa sera ya ushiriki wa wazawa (Local Content) unapaswa kupewa kipaumbele ili kampuni za Kitanzania na wananchi waweze kushiriki katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.

Amesisitiza kuwa kusajili kampuni nchini pekee hakupaswi kuwa kigezo cha kuitambua kuwa ya Kitanzania, bali umiliki wake unapaswa kuzingatiwa ili kuhakikisha fursa zinawanufaisha wazawa.

Ameitaka Wizara ya Nishati kuendelea kuandaa vijana wenye ujuzi unaohitajika na kujenga uwezo wa kampuni za ndani ili ziweze kutoa bidhaa na huduma zinazotumika katika miradi ya mafuta na gesi.

Aidha, amesema utekelezaji wa miradi hiyo unahitaji usimamizi madhubuti, nidhamu katika matumizi ya fedha na uwajibikaji. Kituo cha umahiri kinachopangwa kuanzishwa na Serikali kinatarajiwa kusaidia kukuza ujuzi wa wataalamu wa ndani.

Kuhusu leseni hizo, Ndejembi amesema ni hatua ya kuimarisha utafutaji wa mafuta na gesi nchini, kujenga uwezo wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kufungua fursa za ushirikiano na wawekezaji.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa shughuli za utafutaji na uendelezaji wa rasilimali hizo kupitia TPDC na wadau wengine.

Kuhusu mradi wa gesi asilia iliyopozwa na kuwa kimiminika (LNG) unaotarajiwa kutekelezwa mkoani Lindi, Ndejembi amesema Serikali imekamilisha maandalizi yake na inasubiri wabia pamoja na kampuni za kimataifa kukamilisha hatua zilizobaki ili mradi huo uendelee.

Naye Mkurugenzi wa Utafutaji, Uendelezaji na Uzalishaji wa TPDC, Paschal Njiko, amesema leseni zote nne zinasimamiwa na shirika hilo, ambalo litakuwa na nafasi ya kukaribisha wawekezaji kwa ajili ya shughuli za utafutaji.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Dk. Juma Zuberi Homera, amesema utoaji wa leseni hizo unazingatia Sheria ya Petroli ya mwaka 2015, inayowezesha TPDC kumiliki vitalu vyake na kushiriki moja kwa moja katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia.

Homera amesema Serikali itaendelea kusimamia sekta hiyo kwa kuzingatia sheria, usalama, utunzaji wa mazingira na maslahi ya Taifa, kwa kushirikiana na TPDC, Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na wadau wengine.

Ameeleza pia kuwa uchimbaji wa visima vitatu katika kitalu cha Mnazi Bay, mkoani Mtwara, umekamilika. Visima viwili ni vya uzalishaji na kimoja ni cha utafiti.

Wakati huo huo, takwimu za hadi Septemba 2026 zinaonesha kuwa Tanzania ilikuwa na vituo 22 vya CNG vinavyotoa huduma, karakana 20 za kufunga mifumo ya gesi katika vyombo vya moto na zaidi ya vyombo vya moto 20,000 vinavyotumia gesi hiyo. Viwanda 57, taasisi 31 na takribani kaya 3,000 vilikuwa vimeunganishwa na miundombinu ya gesi asilia.

Serikali imesema inalenga kuhakikisha maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi yanachangia ajira, mafunzo, ujuzi wa wataalamu wa ndani na fursa za kibiashara kwa kampuni za Kitanzania.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments