HomeBiasharaMingle yafungua fursa za biashara kwa wabunifu wa maudhui

Mingle yafungua fursa za biashara kwa wabunifu wa maudhui

📌Mingle yawakutanisha Wabunifu wa Maudhui na Chapa kujadili Thamani ya Kibiashara ya Sekta ya Ubunifu

Kupitia hafla yake ya kwanza, “The Influence Room”, Mingle imewakutanisha wabunifu wa maudhui, chapa na wadau wa sekta kujadili namna ushawishi unavyoweza kuunda utamaduni, kuchochea masoko na kujenga tasnia endelevu ya ubunifu wa maudhui nchini Tanzania.

DAR ES SALAAM, TANZANIA: Mingle, jukwaa la wabunifu wa maudhui na watu wenye ushawishi lililoanzishwa kuziba mapengo katika uchumi unaokua wa ubunifu wa maudhui na ushawishi nchini Tanzania, limejitambulisha rasmi Ijumaa, tarehe 30 Oktoba 2026, kupitia mkutano wake wa kwanza wa wadau wa tasnia, The Influence Room, uliofanyika TABLE 206, Masaki, Dar es Salaam.

Ikiwa na kaulimbiu “Kuunda Utamaduni. Kuchochea Masoko. Kujenga Tasnia,” hafla hiyo iliwakutanisha wabunifu wa maudhui, wawakilishi wa chapa, wataalamu wa matangazo na mawasiliano pamoja na wadau wa sekta ya maendeleo. Washiriki walipata fursa ya kujenga mahusiano, kubadilishana uzoefu na kujadili mabadiliko ya nafasi ya wabunifu wa maudhui katika biashara, utamaduni na jamii.

Kiini cha hafla hiyo kilikuwa The Influence Dialogue, mjadala wa jopo ulioangazia fursa na changamoto zinazoukabili uchumi wa ubunifu wa maudhui Tanzania. Mjadala huo ulihusisha namna wabunifu wanavyoweza kujenga taaluma endelevu, jinsi chapa zinavyoweza kunufaika zaidi na ushirikiano na watu wenye ushawishi, pamoja na hatua zinazohitajika kujenga tasnia yenye kuaminika, mifumo iliyo wazi na uwezo wa kujiendesha kibiashara.

Jopo hilo lilijumuisha mitazamo kutoka kwa wadau mbalimbali wa tasnia, likiwahusisha Godfrey Rwechungura na Atu Bohela wakiwakilisha wabunifu wa maudhui; Martha Silayo wa Bonite Bottlers akiwakilisha chapa; Bruce Mugaisi wa HESA Africa akiwakilisha wakala wa matangazo; na Zainab Mkwepo (Ola), Mwanzilishi Mwenza wa Mingle. Mjadala uliongozwa na Agnes Kabissa wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Mazungumzo yalisisitiza umuhimu wa kupanua namna ushawishi unavyopimwa, kutoka kuangalia idadi ya wafuasi, alama za kupenda na kuonekana pekee, hadi kutambua thamani pana ambayo wabunifu huleta kupitia uaminifu wa hadhira, uhusiano wao na utamaduni, ushirikishwaji wa jamii na uwezo wa kuathiri tabia za watumiaji.

Akizungumzia kujitambulisha kwa Mingle na sababu za kuanzishwa kwake, Zainab Mkwepo (Ola), Mwanzilishi Mwenza wa Mingle, alisema:

“Uchumi wa ubunifu wa maudhui nchini Tanzania una uwezo mkubwa sana, lakini bado kuna pengo kati ya fursa zilizopo kwa wabunifu na mifumo inayohitajika kuifanya tasnia hii kuwa endelevu. Mingle inalenga kusaidia kuziba pengo hilo kwa kuwaunganisha wabunifu na chapa, kuwezesha fursa zenye utaratibu ulio wazi na kuunga mkono ushirikiano unaotambua thamani wanayoleta wabunifu. The Influence Room ni mwanzo wa mazungumzo mapana kuhusu kile tunachoweza kujenga pamoja kama tasnia.”

Hafla hiyo pia ilijumuisha hotuba kuu iliyotolewa na Henry Esiaba, Mkurugenzi wa Masoko na Ubunifu wa Serengeti Breweries Limited (SBL), aliyeshiriki mtazamo wa chapa kuhusu mambo ambayo biashara huzingatia zinaposhirikiana na watu wenye ushawishi. Alisisitiza umuhimu wa wabunifu kuoanisha majukwaa yao, mikakati ya maudhui na namna wanavyoshirikisha hadhira na malengo halisi ya biashara. Alieleza kuwa ushirikiano wenye matokeo unapaswa kutoa thamani inayozidi kufikia hadhira na kuonekana pekee.

Kadiri uchumi wa ubunifu wa maudhui unavyoendelea kukua, umuhimu wa kuimarisha uhusiano kati ya wabunifu na chapa, kuweka makubaliano ya kibiashara yaliyo wazi, kuhakikisha malipo ya haki na kuboresha namna ya kupima matokeo ya kampeni unazidi kuongezeka.

Kupitia jukwaa lake, Mingle inalenga kuimarisha uhusiano ndani ya mfumo wa ubunifu wa maudhui kwa kuwaunganisha wabunifu na chapa, kuwezesha ushirikiano wenye manufaa na kusaidia maendeleo ya kitaaluma pamoja na ukuaji wa kibiashara wa wabunifu. Dhamira yake ni kusaidia kubadilisha uuzaji kupitia watu wenye ushawishi, kutoka ushirikiano unaojikita zaidi katika malipo kwa kampeni moja moja, kuelekea ushirikiano wenye mifumo iliyo wazi, uwazi wa makubaliano na uendelevu.

The Influence Room inaashiria mwanzo wa jitihada za Mingle za kujenga jukwaa la mazungumzo endelevu ya tasnia, ushirikiano na kubadilishana maarifa, likiwakutanisha wanaounda utamaduni na biashara zinazowekeza katika ushawishi wake.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments