Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian, ameagiza kusitishwa kwa shughuli zote za kilimo, ujenzi na uendelezaji katika eneo lenye mgogoro wa ardhi wa Shamba la Serikali la Utafiti na Mifugo Mivumoni, Wilaya ya Pangani, huku TAKUKURU ikiagizwa kuchunguza namna maeneo ya shamba hilo yalivyogawiwa kwa wananchi.
Hatua hiyo inalenga kutatua mgogoro wa muda mrefu wa uvamizi wa shamba hilo linalosimamiwa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambao unahusisha baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Kigurusimba.
Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho Novemba 3, 2026, Dkt. Batilda amesema Serikali itafanya uhakiki wa mipaka ya shamba hilo kwa kutumia ndege nyuki (drone) kupata picha za eneo, kabla ya wataalamu kuweka alama za mipaka na kubaini majengo yaliyopo ndani na nje ya eneo la shamba.
Pia ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza mchakato wa ugawaji wa maeneo hayo ili kubaini kama kulikuwa na vitendo vya rushwa au ukiukwaji wa taratibu, akisisitiza kuwa waliohusika kusababisha mgogoro huo watachukuliwa hatua.
“Namaliza kikao hiki naachia kazi TAKUKURU. Wapitie wote waliopata haya maeneo na wajue kitu gani kilitokea na kama kulikuwa na rushwa katika upatikanaji wa eneo. Waliosababisha hali hiyo ni lazima tuwachukulie hatua,” amesema.




Ametoa pia agizo la kusitisha shughuli zote za uendelezaji hadi zoezi la uhakiki litakapokamilika, akiwataka wananchi kutohamia maeneo mengine ya shamba kabla ya kufanyika kwa upangaji rasmi kwa kutumia ramani.
“Katazo la uendelezaji wa aina yoyote, iwe ni kilimo, iwe ni ujenzi, nawaomba sana yote yasimamishwe. Lakini mtu asiende akaamua kuhamia kwenye eneo lililobaki kabla hajapangwa, kwa sababu unaweza ukaja kuondolewa. Haya mambo yanapangwa kupitia ramani,” amesema.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TVLA, Dkt. Stella Bitanyi, amesema wakala huo uko tayari kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Tanga kutatua mgogoro huo, ikiwemo kushiriki katika uhakiki wa wananchi waliopo ndani na nje ya mipaka ya shamba.
Amesema wataalamu wa TVLA watashirikiana na timu itakayoundwa kubaini maeneo yatakayobaki kwa shughuli za taasisi hiyo, zikiwemo za ufugaji na kilimo cha malisho, huku wakala huo ukikubaliana na hatua za kuanza kazi hiyo katika wiki inayoanza Novemba 9, 2026.
“Ni mgogoro wa muda mrefu, na imekuwa ni mawasiliano ya muda mrefu kutatua hili. Tuko tayari kushirikiana katika kuona kwamba mgogoro huu unaisha na wananchi wanaishi salama. Tunaafiki kuundwa kwa kamati na tuko tayari kuanza kazi wiki inayoanza tarehe 9 Novemba, kupitia na kuona ni nani aliyeko ndani, ni nani aliyeko nje na wapi tunaweka alama za mipaka,” amesema Dkt. Bitanyi.




TVLA imethibitisha kuwa imekubali kuachia hekta 1,271 kati ya hekta 5,320 za shamba hilo kwa Serikali ya Kijiji cha Kigurusimba kwa ajili ya kuwagawia wananchi, huku maeneo mengine yakibaki kwa shughuli za taasisi hiyo.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Rashid Kassim Mchatta, amesema timu ya wataalamu itakayoundwa itahusisha Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi, Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na TVLA.
Amesema timu hiyo itatekeleza maelekezo ya Serikali kwa kufanya uhakiki wa mipaka, upimaji wa maeneo na kushughulikia masuala ya hati za ardhi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigurusimba, Silvesta Mango, amekiri kuwa baadhi ya wananchi wanaishi ndani ya eneo la shamba hilo baada ya kugawiwa maeneo na Serikali ya Kijiji, huku akiiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kubakiza sehemu ndogo ya makazi yaliyopo Kitalu Namba Nne.
Amesema eneo hilo tayari lina nyumba na miundombinu muhimu, ikiwemo umeme, hivyo kuomba wananchi walioishi hapo kwa muda mrefu wazingatiwe katika utatuzi wa mgogoro huo.
Naye mmoja wa wananchi, Mama Mnyetama, ameiomba Serikali kusaidia kupima na kuweka alama za mipaka katika maeneo yao yaliyo nje ya shamba hilo ili kupata uhakika wa umiliki na kuepusha migogoro mingine ya ardhi.
Amesema utambuzi na uwekaji wa alama za mipaka utawasaidia wananchi kuthibitisha uhalali wa maeneo yao na kuendesha shughuli zao za kiuchumi na kijamii kwa utulivu.





