HomeElimuIAA: AI isitumiwe kufanya kazi za wanafunzi

IAA: AI isitumiwe kufanya kazi za wanafunzi

WATAALAMU wa kada mbalimbali wametakiwa kujifunza na kutumia teknolojia ya akili unde (AI) kuboresha utendaji wa majukumu yao, huku walimu na wahadhiri wakihimizwa kubuni mbinu mpya za ufundishaji na tathmini zitakazohakikisha wanafunzi wanaitumia teknolojia hiyo kujifunza badala ya kuwafanyia kazi zao za kitaaluma.

Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Profesa Eliamani Sedoyeka, katika kongamano la kitaaluma lililoandaliwa na chuo hicho na kuwashirikisha wanafunzi wa shahada ya uzamili, wanataaluma na wadau mbalimbali.

Kongamano hilo limejadili changamoto zinazoikabili jamii na namna ya kuzitatua kupitia tafiti na maarifa ya kitaaluma, huku matumizi ya AI yakiwa miongoni mwa masuala yaliyopewa uzito.

Profesa Sedoyeka amesema mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea duniani hayawezi kuzuiliwa, hivyo wataalamu wanapaswa kujifunza namna ya kutumia AI katika kuboresha utendaji na kuongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi.

Amesema ni muhimu kwa walimu, wahadhiri na wataalamu wa kada nyingine kupata mafunzo yatakayowawezesha kuelewa matumizi ya teknolojia hiyo kulingana na mahitaji ya fani zao.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo yanaweza kupatikana kupitia majukwaa ya mtandaoni, yakiwemo Google na Microsoft, ambayo yana programu na kozi zinazowasaidia watu kujifunza matumizi ya AI.

Aidha, amesema kuna mpango wa kutoa mafunzo ya akili unde bila malipo kwa wataalamu na wanafunzi ili kuongeza uelewa na kuwajengea uwezo wa kutumia teknolojia hiyo katika shughuli zao.

Akizungumzia matumizi ya AI katika elimu ya juu, Profesa Sedoyeka amesema teknolojia hiyo inaweza kusaidia wanafunzi na watafiti kubaini maeneo ambayo tayari yamefanyiwa utafiti na yale ambayo bado yana mapengo ya maarifa yanayohitaji kuchunguzwa.

Amesema uwezo huo unaweza kurahisisha upatikanaji wa taarifa za kitaaluma na kuwasaidia watafiti kutambua maeneo mapya ya kufanyia uchunguzi, hivyo kuongeza ufanisi katika mchakato wa utafiti.

Hata hivyo, ameeleza kuwa changamoto inajitokeza pale wanafunzi wanapotumia AI kufanya kazi zao na kuwasilisha matokeo kana kwamba wamezifanyia wenyewe, bila kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu maudhui wanayowasilisha.

Amesema matumizi ya namna hiyo yanaweza kudhoofisha malengo ya elimu, ambayo ni kuwajengea wanafunzi maarifa, ujuzi na weledi, pamoja na kuwasaidia kubadili tabia.

Kutokana na hali hiyo, amewataka walimu na wahadhiri kubuni mbinu mpya za kutoa kazi na kuandaa mitihani zitakazopima uelewa na uwezo halisi wa wanafunzi, hata wanapotumia teknolojia hiyo.

Ametoa mfano wa mwanafunzi anayejifunza kuandaa taarifa za kihasibu, ikiwemo mizania (Balance Sheet), akisema siyo tatizo kutumia AI kupata mwongozo wa namna ya kuandaa nyaraka hizo, mradi aweze kuelewa hatua zinazohusika na kuzitengeneza mwenyewe.

Amesisitiza kuwa tatizo ni pale mwanafunzi anapotumia teknolojia hiyo kuwafanya walimu waamini ana maarifa na uwezo ambao kwa uhalisia hana.

Kwa upande wake, mhitimu wa Shahada ya Uzamili ya Uongozi na Utawala Bora kutoka IAA, Sharfani Zuberi, amewataka wanafunzi, hususan wa vyuo vikuu, kuepuka matumizi mabaya ya AI katika kufanya tafiti na kuandika kazi za kitaaluma.

Zuberi amesema pamoja na teknolojia hiyo kuwa na uwezo wa kurahisisha majukumu mbalimbali, wanafunzi wanapaswa kutumia maarifa na uwezo wao binafsi katika kujifunza, kuandika makala na kuchapisha tafiti ili kulinda ubora na uadilifu wa taaluma.

“Naomba wanafunzi waache kutumia AI kwa namna hasi, kwa sababu taaluma haina udanganyifu. Tujaribu kutumia akili zetu darasani, tunapoandika makala na tunapochapisha tafiti zetu,” amesema.

Ameongeza kuwa baadhi ya mazingira ya kitaaluma yanatumia programu za kuchunguza matumizi ya AI katika kazi zinazowasilishwa, akieleza kuwa hatua hiyo inaweza kuwasaidia wanafunzi kuwajibika zaidi katika kazi zao.

Katika utafiti aliouwasilisha kwenye kongamano hilo, Zuberi amesema alichunguza nafasi ya mawasiliano kati ya menejimenti na wafanyakazi, akieleza kuwa mawasiliano ni nyenzo muhimu katika kufanikisha malengo ya taasisi.

Naye mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili ya Mipango na Usimamizi wa Miradi katika IAA, Imtihal Salem Taufik, amesema AI imemsaidia katika utafiti wake unaohusu matumizi ya teknolojia kufuatilia mwenendo wa magari na watu barabarani katika nyakati tofauti za siku.

Amesema utafiti huo unalenga kuchunguza namna teknolojia inavyoweza kusaidia kufuatilia mwendo wa magari makubwa na madogo, pamoja na kuboresha udhibiti wa taa za barabarani ili kurahisisha usafiri na kupunguza changamoto za msongamano.

Hata hivyo, amesema changamoto mojawapo aliyokutana nayo ni kupata taarifa kutoka kwa baadhi ya wadau, wakiwemo wanajamii na wahandisi, kutokana na tofauti ya uelewa kuhusu masuala ya teknolojia yanayohusiana na utafiti huo.

Ameeleza kuwa AI imemsaidia kupata taarifa na mifano ya namna nchi nyingine, zikiwemo za ukanda wa Afrika Mashariki, zilivyokabiliana na changamoto zinazofanana, hivyo kumpa mawazo ya namna ya kutafuta suluhisho kwa kushirikisha wadau.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments