Tanzania inatarajia kujenga Chuo Mahiri cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (DTI) jijini Dodoma kwa gharama ya Sh bilioni 441.12, kupitia mkopo nafuu kutoka Korea Kusini, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji wa wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu katika teknolojia za kidijiti, ikiwemo Akili Unde (AI).
Mradi huo unafadhiliwa kwa mkopo wa dola za Marekani milioni 167.4 kutoka Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Korea (EDCF), kupitia Benki ya Exim ya Korea Kusini.
Hatua ya utekelezaji wa mradi imefikiwa baada ya Serikali ya Tanzania na benki hiyo kutia saini mkataba wa mkopo Novemba 3, 2026, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Natu El-Maamry Mwamba, amesema chuo hicho kitakuwa na mchango mkubwa katika kuandaa wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu katika fani za kiufundi na kuimarisha sekta ya TEHAMA nchini.
Amesema chuo hicho kitakuwa na vituo vya kisasa vya mafunzo, maabara, miundombinu ya kidijiti na tafiti, pamoja na kuimarisha uhusiano kati ya taasisi za elimu na sekta ya viwanda.

Ameeleza kuwa ushirikiano huo utasaidia kupunguza pengo la ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na kuchochea maendeleo ya teknolojia nchini.
“Mradi huu umekuja wakati mwafaka ambapo Tanzania inaendelea kutekeleza ajenda ya mageuzi ya kidijiti na kujenga rasilimali watu pamoja na uwezo wa kitaasisi unaohitajika kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijiti,” amesema Dk. Mwamba.
Amesema Wizara ya Fedha itashirikiana kwa karibu na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na taasisi nyingine zinazohusika na utekelezaji wa mradi huo, ikiwemo kuhakikisha mchango wa ndani wa Serikali unapatikana ili kuwezesha utekelezaji wenye ufanisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Mwandamizi wa Benki ya Exim ya Korea, Dong-Hoon Lee, amesema mradi huo una umuhimu wa kipekee kwa nchi hizo mbili kwa kuwa ni wa kwanza kuidhinishwa chini ya EDCF mwaka huu na wa kwanza unaohusisha usaidizi katika eneo la Akili Unde.

Amesema majadiliano ya kuidhinisha mradi huo yalianza Aprili mwaka huu, yakafuatiwa na kutolewa kwa sera ya usaidizi wa Serikali mwezi Agosti, kabla ya kufikiwa kwa hatua ya kusaini mkataba Novemba.
Lee amesema kasi ya kufikia makubaliano hayo imetokana na ushirikiano thabiti kutoka Serikali ya Tanzania, huku akieleza kuwa Korea Kusini itaendelea kuwa mshirika wa kuaminika katika kusaidia maendeleo ya nchi kupitia miradi ya pamoja.
Amezitaja sekta za barabara, nishati na afya kuwa miongoni mwa maeneo ambayo nchi hiyo imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Ushirikiano huu utaimarisha ukuaji wa pande zote mbili na urafiki wa nchi hizi mbili,” amesisitiza.
Mradi wa Chuo Mahiri cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Dodoma unaongezeka katika orodha ya miradi inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Benki ya Exim ya Korea, yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.12.
Miradi hiyo inahusisha sekta za nishati, kilimo, maji safi na maji taka, reli na maeneo mengine ya maendeleo.





