Tanzania imewasilisha hatua ilizochukua kuimarisha ulinzi na utekelezaji wa haki za binadamu, ikieleza mageuzi katika sekta ya sheria na haki, demokrasia, utawala bora, usawa wa kijinsia na upatikanaji wa huduma za kijamii.
Hatua hizo zimewasilishwa katika Kikao cha Nne cha Tathmini ya Hali ya Haki za Binadamu kwa Mataifa (Universal Periodic Review – UPR), kinachofanyika katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa jijini Geneva, Uswisi.
Katika wasilisho hilo lililofanyika Novemba 5, 2026, Tanzania imeeleza hatua zilizotekelezwa katika kipindi cha tathmini, huku ikisisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha taasisi na mifumo ya utoaji haki na kulinda utu wa kila mtu kwa kuzingatia Katiba, sheria za nchi na wajibu wa kimataifa kuhusu haki za binadamu.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa katika tathmini iliyopita ya mwaka 2021, Tanzania ilipokea mapendekezo 252 kutoka nchi mbalimbali, ambapo ilikubali 187, yakiwemo 20 yaliyokubaliwa kwa sehemu, huku 65 yakikataliwa. Mapendekezo yaliyokubaliwa yamekuwa msingi wa mageuzi na hatua zilizotekelezwa katika kipindi cha taarifa.
Katika eneo la upatikanaji wa haki, Tanzania imeripoti kuwa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imewafikia takribani wananchi milioni 7.9, wakiwemo wanawake zaidi ya milioni nne.
Kampeni hiyo inalenga kuwawezesha wananchi kupata huduma za kisheria na kuondoa vikwazo vinavyotokana na gharama, umbali na ukosefu wa uelewa wa masuala ya sheria.
Aidha, Serikali imetafsiri sheria 446 kwa lugha ya Kiswahili ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za kisheria na kuwawezesha wananchi kuelewa haki na wajibu wao.
Katika kuimarisha utendaji wa Mahakama, Tanzania Bara imepunguza mrundikano wa mashauri kutoka takribani asilimia 10 hadi asilimia tano, huku muda wa wastani wa kumaliza mashauri ukishuka kutoka siku 95 hadi 66.
Kwa upande wa Zanzibar, mrundikano wa mashauri umepungua kutoka asilimia 43 hadi 18.
Matumizi ya teknolojia katika utoaji haki nayo yamechangia kuhitimishwa kwa mashauri zaidi ya 170,000 kupitia mifumo ya mahakama za kidijitali na vikao vya mtandaoni.




