HomeHabariProfesa Gurumo aitangaza Tanzania Kimataifa, kupitia Sekta ya Bahari

Profesa Gurumo aitangaza Tanzania Kimataifa, kupitia Sekta ya Bahari

TANZANIA imeendelea kupata heshima kimataifa kupitia mchango wa wataalamu wake katika sekta ya bahari baada ya Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Profesa Tumaini Shabani Gurumo, kutunukiwa tuzo ya heshima ya Mwanafunzi wa Zamani Mashuhuri (Outstanding Alumna Award) na Chuo Kikuu cha World Maritime University (WMU), kilichopo nchini Sweden.

Tuzo hiyo imetolewa kutambua mchango wake katika kuimarisha uongozi, elimu na mafunzo ya sekta ya bahari, pamoja na kuchochea maendeleo ya taasisi zinazohusika na sekta hiyo barani Afrika.

Profesa Gurumo alikabidhiwa tuzo hiyo Oktoba 31 mwaka huu na Katibu Mkuu wa Shirika la Bahari Duniani (IMO), Arsenio Dominguez, wakati wa mahafali ya 43 ya WMU yaliyofanyika nchini Sweden, yakihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chuo hicho na Jiji la Malmo.

Kwa zaidi ya miaka 20 aliyotumikia sekta ya bahari, Profesa Gurumo amekuwa na mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko chanya kupitia uongozi, utafiti, ufundishaji na kuimarisha uwezo wa wataalamu katika sekta hiyo.

Katika kipindi hicho, ametumikia kwa miaka 10 katika nafasi mbalimbali za usimamizi na uongozi, huku akifundisha sheria za bahari kwa wataalamu wenye uzoefu na wanaoanza taaluma katika maeneo ya bandari, usafirishaji wa majini na masuala ya bahari.

Akizungumzia mchango wake, Rais wa WMU, Profesa Maximo Mejia Jr, amesema Profesa Gurumo ametumia sehemu kubwa ya maisha yake ya kitaaluma kuendeleza sekta ya bahari kupitia ufundishaji, utafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu.

Amesema juhudi zake zimechangia kuboresha elimu na mafunzo ya sekta hiyo, hatua iliyosaidia kuimarisha viwango vya ubora na kuongeza idadi ya wataalamu wenye ujuzi wa kutekeleza majukumu yao katika meli, bandari na mamlaka za usimamizi wa bahari na usafirishaji wa mizigo.

Aidha, Profesa Gurumo ni mtafiti na mwandishi wa machapisho mbalimbali, yakiwemo kitabu kinachohusu Uchumi wa Buluu, Fursa na Chachu ya Maendeleo.

Pia amekuwa mshauri wa kitaalamu katika masuala ya uchumi wa buluu na usafirishaji wa majini kwa Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (UNECA) na TradeMark East Africa (TMEA).

Katika safari yake ya elimu, Profesa Gurumo alihitimu Shahada ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Tumaini, Kampasi ya Iringa, mwaka 2004, kabla ya kupata Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Masuala ya Bahari, akibobea katika Sheria na Sera, kutoka WMU mwaka 2007.

Mwaka 2012 alipata Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kimataifa za Bahari kutoka Chuo Kikuu cha Dalian Maritime nchini China.

Katika mahafali hayo, Watanzania wengine wanne walitunukiwa vyeti vya kuhitimu shahada ya uzamili na stashahada katika fani mbalimbali zinazohusiana na sekta ya bahari.

Mafanikio hayo yanatarajiwa kuongeza nguvu katika upatikanaji wa wataalamu wenye ujuzi wa kimataifa, kuimarisha uwezo wa Tanzania katika sekta ya bahari na kuongeza mchango wake katika kukuza uchumi wa buluu barani Afrika.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments