Zaidi ya vijana 3,000 wamepata fursa za ajira kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, huku ongezeko la mahitaji ya mafunzo likionyesha mwamko wa vijana kuchangamkia nafasi zinazotokana na mfumo huo.
Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imesema inaendelea kuimarisha mfumo huo ili kuongeza fursa za ajira kwa vijana, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, kuhusu taasisi za Serikali kuweka mipango madhubuti ya kuongeza ajira.
Maagizo hayo yalitolewa hivi karibuni jijini Arusha wakati wa Mkutano wa Watendaji Wakuu wa Taasisi za Serikali, ambapo Makamu wa Rais alizitaka taasisi kuhakikisha zinaweka mikakati ya kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu mchango wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika utekelezaji wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025 na Marejeo ya Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Mwaka 2003, Toleo la Mwaka 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Asangye Bangu, amesema mfumo huo umekuwa chanzo cha ajira kwa vijana katika maghala mbalimbali nchini.
Amesema vijana hao wanashiriki katika shughuli za upokeaji, uhifadhi, upimaji na usimamizi wa bidhaa ghalani, hatua inayoongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.
Bangu amesema pia kumekuwa na ongezeko la vijana wanaojitokeza kushiriki mafunzo yanayowawezesha kupata ujuzi wa kufanya kazi katika maghala yanayotumia mfumo huo.
“Awali tulikuwa tunapata washiriki kati ya 15 hadi 20 katika mafunzo haya, lakini sasa idadi imeongezeka hadi kufikia vijana 150 wanaohudhuria mafunzo kwa wakati mmoja. Hii inaonesha namna vijana wanavyozidi kutambua fursa zilizopo katika Mfumo wa Stakabadhi za Ghala,” amesema.
Ameeleza kuwa WRRB itaendelea kuimarisha mafunzo na kuhamasisha vijana kutumia fursa zinazotokana na kupanuka kwa matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika sekta mbalimbali.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mchango wa bodi katika juhudi za Serikali za kuongeza ajira na kukuza uchumi wa wananchi.




