HomeHabariSerikali yawataka watafiti kutafuta majibu ya changamoto za wananchi

Serikali yawataka watafiti kutafuta majibu ya changamoto za wananchi

Serikali imewataka watafiti nchini kuelekeza tafiti zao katika kutafuta majibu ya changamoto zinazowakabili wananchi, hususan kuongeza ajira, uzalishaji, kupanua masoko na kuboresha maisha ya Watanzania.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk. Pius Chaya, amesema tafiti zinapaswa kuwa na matokeo yanayoweza kutumika katika kutatua changamoto za kiuchumi na kuchochea maendeleo ya wananchi.

Akizungumza leo mkoani Dodoma, wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Tano la Kimataifa la Usimamizi wa Biashara na Maendeleo ya Kiuchumi lililoandaliwa na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), amesema ukuaji wa uchumi una maana pale unapoboresha maisha ya Mtanzania wa kawaida.

Amesema mikakati ya maendeleo inapaswa kujenga uchumi shindani na jumuishi unaowezesha wananchi kushiriki na kunufaika kupitia ajira, biashara na shughuli za uzalishaji.

Ameeleza kuwa tafiti zinapaswa kuangazia namna ya kukuza viwanda na kilimo chenye tija, kuongeza thamani ya mazao ndani ya nchi, kupanua ajira vijijini na mijini na kupunguza utegemezi wa kuuza malighafi nje ya nchi.

Katika eneo la rasilimali watu, amesema kuna umuhimu wa kuandaa vijana wenye ujuzi, nidhamu na ubunifu ili waweze kukabiliana na ushindani wa kimataifa.

Ameipongeza TIA kwa kuanzisha kampasi nane katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Singida, Mwanza, Kigoma, Mtwara, Tanga na Zanzibar, akisema upatikanaji wa elimu na mafunzo ni sehemu muhimu ya kuimarisha rasilimali watu nchini.

Aidha, amesema kupambana na umaskini kunahitaji uwekezaji katika elimu, afya, maji, nishati, ulinzi wa jamii na uwezeshaji wa wanawake na vijana kiuchumi.

Akifafanua maeneo ambayo tafiti zinapaswa kupewa kipaumbele, Dk. Chaya amesema ni pamoja na usimamizi na urahisishaji wa biashara, uwekezaji na ushindani, teknolojia na ubunifu.

“Kwenye usimamizi na urahisishaji wa biashara tunahitaji kujua namna ya kupunguza urasimu, gharama za uzingatiaji wa sheria na taratibu na kuongeza ufanisi wa taasisi za udhibiti,” amesema.

Ameongeza kuwa tafiti zinahitajika kubainisha namna ya kuvutia uwekezaji wenye tija, kuongeza mitaji katika sekta za uzalishaji na kuimarisha ushindani wa biashara za ndani.

Kuhusu teknolojia, amesema watafiti wanapaswa kuchunguza namna mifumo ya kidijitali na akili unde (AI) inavyoweza kutumika kuongeza tija na kuboresha usimamizi wa biashara.

Pia, amesisitiza umuhimu wa tafiti zitakazosaidia kuoanisha elimu na mafunzo na mahitaji ya soko la ajira, hususan kwa vijana, pamoja na kuimarisha uzalishaji na masoko.

Amesema nchi inahitaji tafiti zitakazobainisha namna ya kuongeza thamani ya bidhaa, kuimarisha minyororo ya thamani na kupanua masoko ya ndani na nje ya nchi.

Akirejea takwimu za Utafiti Jumuishi wa Nguvu Kazi wa mwaka 2025, amesema kilimo kinaajiri asilimia 54.4 ya watu wote walioajiriwa nchini, hali inayoonesha umuhimu wa kufanya tafiti zitakazoongeza tija ya sekta hiyo, thamani ya mazao na uhusiano kati ya kilimo, viwanda na masoko.

Kuhusu mchango wa sekta binafsi, amesema ina nafasi kubwa katika shughuli za kiuchumi, uzalishaji na ajira, hivyo haiwezekani kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 bila kuwa na sekta binafsi yenye tija na ushindani, inayofanya kazi katika mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji.

Amesema Serikali inaitambua sekta binafsi kama mshirika muhimu katika kujenga uchumi wa taifa, si mdau wa maendeleo pekee.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments