WANAWAKE wanaohudumu katika vyombo vya ulinzi na usalama wameshiriki mjadala katika Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Wabunge Wanawake wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR), unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Walioshiriki mjadala huo ni Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Kamishna Mstaafu wa Polisi (CP) Suzan Kaganda, Mkurugenzi wa Kanda wa AFUTA International Alliance kutoka Kenya, Betty Mutesi, na Mwakilishi wa Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania, Luteni Kanali Shani Masasi.
Mkutano huo umefanyika kuanzia Novemba 2 hadi 5, 2026, ukiwakutanisha wabunge wanawake na viongozi mbalimbali kutoka nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu kujadili nafasi ya wanawake katika kuimarisha amani na maendeleo.
Akifungua mkutano huo, Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, amesema wanawake ni viongozi, wapatanishi na wajenzi wa amani, hivyo kuna umuhimu wa kuondoa mila kandamizi, ubaguzi na vikwazo vya kiuchumi vinavyopunguza ushiriki wao.
Amesema Tanzania inaendelea kuwawezesha wanawake kupitia fursa za uongozi, elimu, masoko, mitaji na mikopo yenye masharti nafuu.
Kwa upande wake, Rais wa Jukwaa la Mabunge la Ukanda wa Maziwa Makuu ambaye pia ni Spika wa Bunge la Angola, Adão de Almeida, amesisitiza umuhimu wa ushiriki kamili wa wanawake katika kujenga amani ya kudumu.
Mkutano huo umehudhuriwa pia na Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu; Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Judith Tuluka; Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Ukanda wa Maziwa Makuu, Huang Xia; pamoja na Rais wa kwanza wa Bunge la Umoja wa Afrika na Katibu Mkuu wa Mkutano wa Beijing wa mwaka 1995, Balozi Dk. Gertrude Mongella.
Viongozi wengine waliohudhuria ni Spika mstaafu, Anne Makinda, maspika, wabunge, mawaziri, mabalozi, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, washirika wa maendeleo na asasi za kiraia.
Kauli mbiu ya mkutano huo ni “Ukanda wa Maziwa Makuu Wenye Amani na Maendeleo.”





