HomeBiasharaOthman aipongeza PSSSF kwa kuboresha huduma kidijitali

Othman aipongeza PSSSF kwa kuboresha huduma kidijitali

Matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma za hifadhi ya jamii yamepunguza usumbufu kwa wanachama, kwa kuwawezesha kupata huduma bila kulazimika kufika mara kwa mara katika ofisi za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

Hayo yamesemwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, Novemba 10, 2026, alipotembelea banda la PSSSF katika maonesho ya Mkutano wa 11 wa Mwaka wa Mtandao wa Wataalamu wa Rasilimali Watu katika Sekta ya Umma Afrika (APS-HRMnet), uliofanyika Zanzibar.

Othman ameipongeza PSSSF kwa kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma, akisema hatua hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanachama na kupunguza gharama na muda unaotumika kufuata huduma hizo.

Makamu huyo wa Rais, aliyemwakilisha Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi katika ufunguzi wa mkutano huo, amepata maelezo kuhusu huduma za Mfuko kutoka kwa Meneja wa PSSSF Ofisi ya Zanzibar, Mariam Saleh.

Mariam amemweleza namna PSSSF unavyoendelea kuboresha mifumo yake ili kuongeza ufanisi, ambapo huduma mbalimbali sasa zinapatikana kwa njia ya kidijitali, hatua inayolenga kuwawezesha wanachama kuzifikia kwa urahisi zaidi.

Aidha, Othman ameelezwa kuhusu kaulimbiu mpya ya Mfuko isemayo “Tunalipa Jana”, inayosisitiza dhamira ya kuhakikisha wanachama wanapata mafao yao kwa wakati na kwa ufanisi.

Dhamira hiyo pia inahusisha kuimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa michango ya wanachama ili kuwezesha ulipaji wa mafao kwa wakati.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments