Serikali na Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), wamekubaliana kuendeleza ushrikiano katika kutatua changamoto mbalimbali za wenye viwanda nchini.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo wakati Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho hilo Mhandisi Benedict Lema, akiambatana na Mkurugenzi Mtendaji aliyemaliza muda wake, Leodegar Tenga, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji mpya, Frank Dafa, walipofanya mkutano rasmi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Salum.
Ujumbe wa CTI ulimtambulisha rasmi Mkurugenzi Mtendaji mpya, Frank J. Dafa, na kutoa shukrani za dhati kwa Katibu Mkuu kwa kukubali mwaliko wa kuwa Mgeni Rasmi katika Mkutano Mkuu wa 33 wa Mwaka wa Wanachama wa CTI utakaofanyika tarehe 10 Desemba 2026, na kutanguliwa na Kongamano la Viwanda, Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, CTI iliishukuru Wizara na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais DKt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada endelevu za kukuza na kuendeleza viwanda nchini.
Akiwasilisha hoja na changamoto mbalimbali zinazoathiri ufanisi wa wazalishaji wa ndani, Dafa alisisitiza umuhimu wa kuimarisha uratibu wa kisera na maamuzi ili kuondoa vikwazo vya kiutendaji na kodi. Pande zote zilikubaliana kuendelea kuimarisha majukwaa ya mazungumzo kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPD) ili kupata suluhisho la pamoja na la kudumu.
Kwa CTI, mazungumzo haya yanadhihirisha madhumuni yetu ya kuendeleza juhudi za kutetea maslahi ya viwanda, kuhakikisha kero za viwanda zinasikilizwa, na kupatiwa majawabu ya kimkakati.







