BENKI ya NMB imeibuka na tuzo tatu katika hafla ya Tanzania Marketing Awards 2026 (TMA2026) iliyofanyika Novemba 13, 2026, ikitambuliwa kwa ubunifu na mafanikio ya kampeni zake za masoko zinazolenga makundi mbalimbali ya wateja.
Katika tuzo hizo, NMB ilishinda kipengele cha Best Banking & Financial Services Marketing Campaign kupitia kampeni ya Mkononi Patamu, huku kampeni yake ya SME Spend Campaign ikitwaa tuzo ya Best SME Marketing Campaign, inayotambua kampeni za masoko zinazolenga biashara ndogo na za kati.
Benki hiyo pia ilitwaa tuzo ya Best Experiential Marketing Campaign kupitia Kariakoo Festival 2026, iliyotekelezwa kwa ushirikiano na One Voice Events. Ushindi huo umeifanya NMB kutambuliwa katika maeneo matatu tofauti ya masoko, yakiwemo huduma za kifedha, biashara ndogo na za kati pamoja na kampeni zinazowashirikisha wateja moja kwa moja.
Kupitia taarifa yake, NMB imeeleza kuwa tuzo hizo ni heshima kwa wateja, wadau na wafanyakazi wake wanaoendelea kuchangia mafanikio ya kampeni za benki hiyo. Aidha, imewashukuru wateja kwa kuendelea kuiamini, huku ikisisitiza dhamira yake ya kubuni kampeni zinazokidhi mahitaji yao na kuleta matokeo chanya.







