Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius John Ndejembi, ameliagiza Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi (NEEC) kusimamia mchakato wa kuunganisha mifuko na programu 75 za uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kuunda mfuko mmoja utakaorahisisha upatikanaji wa mitaji na dhamana kwa wananchi.
Amesema mfumo huo mpya unapaswa kuzingatia mahitaji ya sasa ya wananchi, hususan vijana wenye mawazo ya biashara na miradi ya uzalishaji, ambao wanakosa sifa za kupata mikopo katika taasisi nyingine za fedha.
Makamu wa Rais ametoa agizo hilo wakati wa maadhimisho ya mwaka mmoja wa Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, alipokuwa akipokea taarifa ya majukumu ya NEEC.
Amesema kuunganishwa kwa mifuko hiyo kunapaswa kusaidia kupunguza vikwazo vya upatikanaji wa mitaji, kutoa dhamana kwa wanaohitaji mikopo na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za kiuchumi nchini.
Katika taarifa hiyo, Katibu Mtendaji wa NEEC, Jabiri Makame, amesema baraza hilo ni chombo cha kitaifa chenye jukumu la kusimamia, kufuatilia na kuratibu shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Amesema majukumu hayo yanajumuisha kuratibu upatikanaji wa mitaji na masoko, kusimamia mifuko na programu za uwezeshaji, kuwezesha ukuaji wa biashara zinazomilikiwa na Watanzania pamoja na kuratibu utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa ushiriki wa Watanzania katika shughuli za kiuchumi.
Ameeleza kuwa mkakati huo unahusisha shughuli zinazotekelezwa na wizara za kisekta, taasisi za umma na sekta binafsi.




