HomeBiasharaTanzania kushiriki mjadala wa ufadhili endelevu wa Afrika

Tanzania kushiriki mjadala wa ufadhili endelevu wa Afrika

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ameongoza ujumbe wa Tanzania uliowasili Paris, Ufaransa, kushiriki Jukwaa la 25 la Kimataifa la Uchumi Afrika litakalojadili changamoto za madeni na upatikanaji wa ufadhili wa maendeleo kwa nchi za Afrika.

Jukwaa hilo linatarajiwa kufanyika Novemba 25, 2026, katika Kituo cha Mikutano cha Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD), mjini Paris.

Akiwasili nchini humo, Balozi Omar amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Said Othman Yakubu, na kufanya kikao cha kupitia ajenda na maandalizi ya ushiriki wa ujumbe wa Tanzania.

Jukwaa hilo, lenye kaulimbiu “Kufadhili Mabadiliko ya Kiuchumi ya Afrika”, linawakutanisha watunga sera, washirika wa maendeleo, taasisi za ufadhili, wawekezaji na wadau wengine kujadili vipaumbele vya ufadhili wa maendeleo ya bara hilo.

Balozi Omar anatarajiwa kushiriki kama mjumbe wa majadiliano katika jopo la kwanza lenye mada “Kuelekea Upatikanaji wa Deni la Gharama Nafuu na Endelevu kwa Afrika katika Nyakati za Migogoro ya Kimataifa”.

Jopo hilo litajadili namna nchi za Afrika zinavyoweza kusawazisha gharama na vihatarishi vya madeni ya taifa na mahitaji ya fedha kwa ajili ya mabadiliko ya kiuchumi, pamoja na nafasi ya washirika wa kimataifa katika kuwezesha upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu.

Majadiliano ya jukwaa hilo pia yataangazia changamoto za nchi za Afrika katika kupata fedha za maendeleo, wakati masharti ya ufadhili yanazidi kuwa magumu, gharama za kulipa madeni zinaongezeka na nafasi ya bajeti za Serikali kutekeleza miradi inapungua.

Wadau wanatarajiwa kujadili mbinu za kupata ufadhili wa gharama nafuu na endelevu, kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kubuni njia mbadala za kugharamia mabadiliko ya kiuchumi.

Aidha, jukwaa hilo litakuwa na uzinduzi wa ripoti ya Africa’s Development Dynamics 2026: Managing Debt for Transformation (Mienendo ya Maendeleo ya Afrika 2026: Kusimamia Deni kwa Mabadiliko), iliyoandaliwa kwa pamoja na Kituo cha Maendeleo cha OECD na Tume ya Umoja wa Afrika.

Ripoti hiyo inatarajiwa kutoa mwongozo kwa nchi za Afrika kuhusu usimamizi wa madeni na namna ya kuhakikisha ufadhili unaelekezwa katika shughuli zinazochochea mabadiliko ya kiuchumi na maendeleo endelevu.

Miongoni mwa wajumbe walioambatana na Waziri wa Fedha ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Asha Khamisi Abdulah, na Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Rished Bade.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments