HomeBiasharaDira 2050: Tanzania yahitaji kizazi cha wabunifu wa teknolojia

Dira 2050: Tanzania yahitaji kizazi cha wabunifu wa teknolojia

Na Manish Govindji, Afisa Mtendaji Mkuu, Liquid Intelligent Technologies Tanzania

Ili Tanzania ifikie azma yake ya kuwa kitovu cha teknolojia na ubunifu katika ukanda ifikapo mwaka 2050, kupanua miundombinu ya kidijitali pekee hakutatosha. Nchi pia inahitaji kujenga kizazi chenye uwezo wa kubuni teknolojia, kuanzisha biashara, kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi na kuzalisha ajira kupitia ubunifu.

Wakati Rais Samia Suluhu Hassan alipozindua nyenzo za utekelezaji, ufuatiliaji na kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Agosti 3, msisitizo kuhusu ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ulionyesha nafasi muhimu ya uwekezaji wa sekta hiyo katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya nchi.

Inakadiriwa kuwa takribani asilimia 70 ya utekelezaji wa Dira ya 2050 utatokana na sekta binafsi. Hali hiyo inaweka wajibu mkubwa kwa kampuni za teknolojia, si tu kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali, bali pia kusaidia kujenga rasilimali watu yenye ujuzi unaohitajika kuendesha uchumi unaolenga kufikia thamani ya dola za Marekani trilioni moja.

Kuvuka mipaka ya miundombinu

Nafasi kubwa ya sekta binafsi katika kutekeleza Dira ya 2050 inaambatana na wajibu wa kuhakikisha uwekezaji wa teknolojia unaleta matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi. Kwa kampuni za teknolojia kama Liquid Intelligent Technologies Tanzania, jukumu hilo linapaswa kwenda zaidi ya kutoa huduma za mawasiliano na kuwaunganisha watu na mifumo ya kidijitali.

Mabadiliko ya kidijitali hayapimwi tu kwa idadi ya watu wanaopata intaneti, bali pia kwa kile wanachoweza kufanya kupitia muunganisho huo. Swali muhimu ni iwapo teknolojia inawawezesha vijana kubuni bidhaa, kuanzisha biashara, kupata ajira na kutatua changamoto zinazozunguka maisha yao.

Liquid, ambayo ni sehemu ya Cassava Technologies, inahudumia zaidi ya biashara 2,000 nchini Tanzania. Kampuni hiyo inaendesha mfumo jumuishi wa huduma za kidijitali unaojumuisha mawasiliano, vituo vya kuhifadhi na kuchakata data, huduma za kompyuta za mtandaoni (cloud), usalama wa mtandao, suluhisho za Akili Unde (AI) na mifumo ya malipo ya kidijitali.

Hata hivyo, hatua inayofuata kwa Tanzania ni kuimarisha uhusiano kati ya uwekezaji katika miundombinu hiyo na ukuzaji wa vipaji vya ndani. Licha ya maendeleo yaliyofikiwa, baadhi ya maeneo bado yanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa huduma za mawasiliano. Aidha, uwepo mdogo wa watoa huduma wakubwa wa miundombinu ya kompyuta za mtandaoni (hyperscalers) unaweza kuongeza gharama na kupunguza kasi ya matumizi ya teknolojia hizo.

Kwa hiyo, sambamba na kuendelea kupanua miundombinu, Tanzania inahitaji kuvutia washirika wa kimataifa wa teknolojia na wakati huohuo kuimarisha utaalamu wa ndani katika maeneo mbalimbali ya kidijitali.

Miundombinu imara ikiunganishwa na watu wenye ujuzi, biashara zitapata nafasi ya kukua na kupanuka, kuongeza uzalishaji, kutengeneza ajira na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Kujenga kizazi cha wabunifu na wazalishaji

Kukuza vipaji vya kidijitali kunapaswa kwenda mbali zaidi ya mafunzo ya matumizi ya kompyuta na programu za kawaida. Vijana wanahitaji kuandaliwa kuwa wabunifu wa programu na mifumo ya teknolojia, wahandisi, wataalamu wa usalama wa mtandao, wachambuzi wa data na wajasiriamali wa kidijitali.

Muhimu zaidi, wanapaswa kujenga uwezo wa kufanya majaribio, kutambua changamoto zinazohitaji suluhisho, kubuni mawazo mapya na kuendelea kujifunza kadiri teknolojia inavyobadilika.

Ujuzi huo unaweza kuwa msingi wa kuibua biashara mpya zinazotumia teknolojia kutatua changamoto katika sekta kama kilimo, afya, elimu, usafirishaji, fedha na viwanda. Kwa mfano, kijana mwenye ujuzi wa teknolojia anaweza kubuni mfumo unaowaunganisha wakulima na masoko, kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya au kusaidia biashara ndogo kusimamia shughuli zake kwa gharama nafuu.

Hapo ndipo uwekezaji katika elimu ya teknolojia unapoanza kuleta manufaa mapana zaidi ya kuongeza idadi ya watumiaji wa huduma za kidijitali. Unakuwa njia ya kujenga biashara, kuongeza ajira na kuwezesha vijana kushiriki katika uzalishaji wa thamani ndani ya nchi.

Mchango wa Liquid katika eneo hili unajumuisha programu ya ProjeKt Inspire, inayolenga kukuza elimu ya vitendo katika Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) miongoni mwa vijana. Programu hiyo inahusisha shughuli za shuleni, programu za vijana, mafunzo kwa walimu na rasilimali za kujifunzia.

Kampuni hiyo pia inadhamini Tuzo za TEHAMA zinazotambua mafanikio na ubunifu katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano nchini Tanzania. Juhudi hizo zinaweza kusaidia kuibua vipaji, kutambua kazi za wabunifu wa ndani na kuongeza fursa za suluhisho zao kufahamika zaidi.

Hata hivyo, ili mipango ya aina hiyo ilete matokeo ya muda mrefu, inahitaji kuunganishwa na mifumo ya elimu, mafunzo ya ufundi, vyuo vikuu na mazingira ya biashara yanayowezesha vijana kutumia ujuzi wao katika kutengeneza bidhaa na huduma zinazoweza kuuzwa sokoni.

Ushirikiano katika kujiandaa kwa mustakabali wa kidijitali

Kujenga nguvu kazi yenye ujuzi wa teknolojia kunahitaji ushirikiano wa karibu kati ya kampuni za teknolojia, vyuo vikuu, vituo vya ubunifu, taasisi za mafunzo na washirika wa kimataifa.

Programu za vyeti vya kitaaluma, mafunzo kwa vitendo, ulezi wa kitaaluma na majukwaa ya ubunifu zinaweza kuwasaidia vijana kupata uzoefu unaohitajika katika mazingira halisi ya kazi. Pia zinaweza kuunganisha elimu wanayoipata darasani na mahitaji ya soko la ajira.

Ushirikiano huo ni muhimu kwa sababu teknolojia inabadilika kwa kasi, huku mahitaji ya waajiri yakihitaji ujuzi unaoendana na mifumo mipya. Hivyo, vijana wanahitaji fursa za kujifunza kwa vitendo na kuendelea kuboresha uwezo wao hata baada ya kumaliza masomo rasmi.

Kutambua ubunifu unaofanywa na Watanzania pia ni hatua muhimu katika kubadili mtazamo kuhusu nafasi ya nchi katika uchumi wa kidijitali. Badala ya kutegemea zaidi teknolojia zinazoletwa kutoka nje, Tanzania inahitaji kujenga mazingira ambayo mawazo na suluhisho zinazobuniwa nchini zinaweza kukua, kupata mitaji na kufikia masoko makubwa.

Kwa sasa, watu binafsi na taasisi mbalimbali nchini wanaendelea kubuni suluhisho za kiteknolojia. Changamoto ni kuhakikisha kunakuwa na mifumo inayowezesha mawazo hayo kufanyiwa majaribio, kupata msaada wa kitaalamu na kifedha, kisha kukua na kuwa biashara zenye uwezo wa kuzalisha ajira.

Kwa kampuni za teknolojia, hili linahitaji mtazamo unaovuka utoaji wa miundombinu pekee. Mtandao hauwezi kuanzisha biashara bila watu wenye mawazo na uwezo wa kutumia fursa zake. Vivyo hivyo, huduma za kompyuta za mtandaoni haziwezi zenyewe kuzalisha ubunifu bila wataalamu wanaoweza kuzitumia kutengeneza bidhaa na huduma mpya.

Kwa hiyo, kampuni za teknolojia zinapaswa kushiriki katika kujenga mazingira yatakayowawezesha Watanzania kutumia miundombinu iliyopo kubuni na kuendeleza suluhisho zao wenyewe.

Kutoka kuwa watumiaji hadi wazalishaji wa teknolojia

Ifikapo mwaka 2050, Tanzania ina fursa ya kuwa kitovu muhimu cha teknolojia na ubunifu katika Afrika Mashariki na Kati. Ili kufikia lengo hilo, nchi inahitaji kuongeza uwezo wa kutumia teknolojia katika sekta mbalimbali na kuimarisha mfumo wa ndani wa ubunifu.

Jambo la msingi zaidi ni kuondoka katika nafasi ya kutegemea teknolojia zinazozalishwa nje na kuelekea katika kuzalisha bidhaa, huduma na suluhisho za kidijitali zinazoweza kutumiwa ndani na kuuzwa katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Mabadiliko hayo yanaweza kuongeza ajira, kuvutia uwekezaji na kukuza mchango wa Tanzania katika uchumi wa kidijitali. Pia yatafungua nafasi kwa vijana kushiriki katika biashara za teknolojia, badala ya kubaki watumiaji wa huduma zinazotengenezwa na wengine.

Hata hivyo, mafanikio hayo yatategemea zaidi ya upatikanaji wa miundombinu. Yanahitaji watu wenye ujuzi wa kutosha, mifumo inayowezesha ubunifu, upatikanaji wa mitaji na mazingira rafiki kwa biashara changa kukua.

Kwa sekta binafsi, kuchangia katika kujenga uwezo huo ni sehemu muhimu ya kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya 2050. Kwa Serikali na taasisi za elimu, ni fursa ya kuimarisha uhusiano kati ya elimu, ujuzi na mahitaji ya uchumi unaobadilika.

Lengo la Tanzania halipaswi kuwa kuandaa vijana wanaoweza kutumia teknolojia pekee, bali kujenga kizazi chenye ujuzi, ujasiri na fursa za kubuni teknolojia, kuanzisha biashara na kuzalisha ajira. Huo ndio msingi wa kuwa taifa linaloshiriki kikamilifu katika kuunda mustakabali wa uchumi wa kidijitali ifikapo mwaka 2050.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments