HomeBiasharaTanzania, Ufaransa zasaini mikataba ya Sh bilioni 513

Tanzania, Ufaransa zasaini mikataba ya Sh bilioni 513

Serikali ya Tanzania imeingia mikataba mitatu ya mikopo yenye masharti nafuu ya euro milioni 175, sawa na takriban Sh bilioni 513, na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji na usafi wa mazingira, miundombinu ya chakula, uvuvi na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Mikataba hiyo inalenga kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira katika maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria, kuimarisha miundombinu ya biashara na usambazaji wa chakula katika miji ya Mwanza na Tanga, pamoja na kuongeza uzalishaji wa uvuvi na maziwa kwa wafugaji wadogo.

Mikataba hiyo imesainiwa jijini Paris, Ufaransa, na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, na Mkurugenzi Mkuu wa AFD, Christophe Lecourtier.

Tukio hilo limefanyika katika makao makuu ya AFD, kando ya Jukwaa la 25 la Kimataifa la Uchumi Afrika lililoandaliwa kwa ushirikiano na Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD).

Mkataba wenye thamani kubwa zaidi ni wa euro milioni 90, sawa na Sh bilioni 263.8, unaofadhili Awamu ya Pili ya Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira katika maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria. Mradi huo unalenga kuboresha upatikanaji wa maji safi na huduma za usafi wa mazingira kwa wakazi wa maeneo husika.

Mkataba wa pili wenye thamani ya euro milioni 55, sawa na Sh bilioni 161.2, unahusu Programu ya Uwekezaji Endelevu katika Mifumo ya Chakula Mijini (TASUFIP), inayolenga kuboresha miundombinu inayotumiwa na wafanyabiashara na wadau wa usambazaji wa chakula katika miji ya Mwanza na Tanga.

Mkataba wa tatu, wenye thamani ya euro milioni 30, sawa na Sh bilioni 87.9, unafadhili programu ya kuendeleza sekta ya uvuvi na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kwa wafugaji wadogo, kwa kuzingatia athari za mabadiliko ya tabianchi.

Programu hiyo inafadhiliwa kwa pamoja na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Mfuko wa OPEC na Mfuko wa Tabianchi wa Kijani (GCF), kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi na maziwa, pamoja na kuimarisha uwezo wa wafugaji wadogo kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumzia mikataba hiyo, Balozi Omar amesema mafanikio ya makubaliano hayo yatapimwa kupitia utekelezaji wa miradi na matokeo yake katika kuboresha huduma na maisha ya wananchi.

Amesema wakazi wa maeneo ya Ziwa Victoria wanatarajiwa kunufaika na huduma bora za maji na usafi wa mazingira, huku wafanyabiashara wa chakula Mwanza na Tanga wakitarajiwa kupata miundombinu bora ya kuendesha shughuli zao.

Aidha, amesema wavuvi na wafugaji wadogo wa ng’ombe wa maziwa watanufaika na uwekezaji utakaosaidia kuendeleza uzalishaji licha ya changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Waziri huyo ameishukuru Serikali ya Ufaransa kupitia AFD kwa ushirikiano wa muda mrefu, akisema umejengwa katika misingi ya kuaminiana, malengo ya pamoja ya maendeleo na dhamira ya kuboresha maisha ya wananchi.

Kwa upande wake, Lecourtier amesema Ufaransa kupitia AFD inathamini ushirikiano wa maendeleo na Tanzania na iko tayari kuuendeleza kwa manufaa ya pande zote mbili.

Ameeleza kuwa shirika hilo linaangalia maeneo mengine ya ushirikiano katika miradi ya kimkakati inayoweza kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Mikataba hiyo mipya inafanya thamani ya jumla ya ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na AFD kufikia euro bilioni 1.3, sawa na takriban Sh trilioni 3.81. Fedha hizo zimeelekezwa katika miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii, ikiwamo maji, kilimo, nishati na miundombinu.

Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Saidi Othman Yakubu; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Asha Khamis Abdulla; na Kamishna wa Fedha za Nje wa wizara hiyo, Rished Bade.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments