HomeBiasharaWakulima 9,000 kunufaika na mradi wa iMBEJU

Wakulima 9,000 kunufaika na mradi wa iMBEJU

Wakulima wadogo 9,000, hususan vijana na wanawake, wanatarajiwa kunufaika na mradi wa iMBEJU Kilimo Sasa unaolenga kuwawezesha kuongeza uzalishaji, kipato na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mradi huo wa miaka miwili umeanzishwa na CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na Rabo Foundation, na utatekelezwa katika mikoa ya Mbeya, Iringa na Kagera kwa kuwalenga wakulima wa mahindi, mpunga na maharage.

Kupitia mradi huo, wakulima watanufaika na mitaji, mafunzo ya kilimo cha kisasa, elimu ya fedha, bima na kuunganishwa na masoko ili kuimarisha kilimo biashara.

Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, amesema mpango huo unaendana na Ajenda ya 10/30 na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 katika kuifanya sekta ya kilimo kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi, ajira na uwezeshaji wananchi.

Amesema katika msimu wa kilimo wa 2025/26, uzalishaji wa mazao ya chakula nchini umefikia tani milioni 25.2, na kuwezesha Tanzania kufikia utoshelevu wa chakula wa asilimia 133.

Mweli amesema Serikali iko tayari kushirikiana na taasisi hizo kuratibu huduma za ugani, kutoa mwongozo wa kitaalamu na kupanua wigo wa mradi ili kuwafikia wakulima wengi zaidi.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema mradi huo umetokana na uzoefu wa taasisi hiyo katika kuwawezesha wakulima wadogo, huku akieleza kuwa mafanikio ya kilimo yanahitaji zaidi ya mikopo, bali mfumo unaowaunganisha wakulima na uzalishaji wenye tija, bima na masoko.

Amesema kupitia mradi huo, wanatarajia kuongeza uzalishaji wa mazao kwa asilimia 30 na kipato cha kaya zinazoshiriki kwa asilimia 25, huku wakulima wakihimizwa kutumia mbinu za kilimo himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Programu za Afrika wa Rabo Foundation, Bas Evers, amesema ushirikiano huo unaunganisha utaalamu na rasilimali ili kuwawezesha wakulima wadogo kuongeza ushindani na kujenga mifumo endelevu ya kilimo.

Naibu Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Onno Koopmans, amesema mradi huo unaonesha ushirikiano wa nchi hizo katika kuendeleza kilimo endelevu, kuimarisha usalama wa chakula na kukuza uchumi wa jamii za vijijini.

Utekelezaji wa mradi tayari umeanza mkoani Mbeya, katika wilaya za Mbarali na Kyela pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, ambako mafunzo kwa wakufunzi yamefanyika kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali. Baadaye mradi utapanuliwa katika mikoa ya Iringa na Kagera.

Taarifa za CRDB Bank Foundation zinaonesha kuwa kupitia programu ya iMBEJU Kilimo, taasisi hiyo tayari imewawezesha zaidi ya vijana na wanawake 36,000 katika kilimo na ufugaji mdogo, kwa kutoa mitaji ya zaidi ya Sh bilioni 3.6 na kuchangia uzalishaji wa ajira zaidi ya 10,000 katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023, CRDB Bank Foundation imesema imefikia zaidi ya wajasiriamali wadogo milioni 2.02 na kutoa mitaji wezeshi ya jumla ya Sh bilioni 26 kupitia programu ya iMBEJU.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments