HomeHabariMaafisa Ustawi wa Jamii na TEHAMA wapatiwa mafunzo Dar

Maafisa Ustawi wa Jamii na TEHAMA wapatiwa mafunzo Dar

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Ayoub Kibao, amewataka washiriki wa mafunzo ya ukusanyaji, uhifadhi na usimamizi wa taarifa za watu wenye ulemavu kutekeleza jukumu hilo kwa weledi na umakini ili kuiwezesha Serikali kupanga na kutekeleza kwa ufanisi huduma zinazolenga kuboresha maisha ya kundi hilo.

Dk. Kibao ametoa wito huo leo Juni 10, 2026, wakati akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Mhinte.

Amesema upatikanaji wa taarifa sahihi na za kuaminika kuhusu watu wenye ulemavu ni msingi muhimu wa kupanga sera, huduma na programu za maendeleo zinazokidhi mahitaji halisi ya wananchi hao.

Mafunzo hayo yanawakutanisha Maafisa Ustawi wa Jamii pamoja na Maafisa TEHAMA kutoka halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Dar es Salaam, yakilenga kuwajengea uwezo wa kutumia mfumo wa ukusanyaji, uhifadhi na usimamizi wa taarifa za watu wenye ulemavu.

Dk. Kibao amesema matumizi sahihi ya mfumo huo yataisaidia Serikali kupata takwimu sahihi, kufuatilia mahitaji ya wenye ulemavu na kuboresha utoaji wa huduma katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, ajira na ustawi wa jamii.

Amehimiza washiriki kutumia mafunzo hayo kuongeza ujuzi na maarifa yatakayochangia kuimarisha usimamizi wa taarifa na kuhakikisha hakuna mwenye ulemavu anayeachwa nyuma katika mipango ya maendeleo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments