Kampuni ya huduma za kifedha kwa njia ya simu, Mixx, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe (STCDA) na Kampuni ya Osaju , imezindua rasmi mfumo mpya wa kidigitali wa ukusanyaji wa ada za maegesho ya vyombo vya moto katika maeneo ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Uzinduzi wa mfumo huo unalenga kuboresha ukusanyaji wa mapato ya Mamlaka kwa uwazi, ufanisi na usalama zaidi, huku ukiwarahisishia wananchi kufanya malipo kwa njia za kisasa kupitia simu zao za mkononi. Mfumo huu mpya unawawezesha madereva na wamiliki wa vyombo vya moto kulipa ada za maegesho papo hapo bila kutumia fedha taslimu, huku taarifa za miamala zikionekana kwa wakati halisi na mapato kufikishwa moja kwa moja kwa Mamlaka husika bila upotevu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Meneja wa Biashara wa Mixx Zanzibar, Salum Nassor Mohamed, alisema mfumo huo ni matokeo ya dhamira ya pamoja ya kutumia teknolojia kuboresha maisha ya wananchi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za umma.




“Kupitia ushirikiano huu, wananchi sasa wanaweza kulipa ada za maegesho kwa njia rahisi, salama na ya uwazi kupitia simu zao za mkononi. Hii ni hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali huku ikirahisisha maisha ya wananchi,” alisema Salum.
Akifafanua namna ya kufanya malipo hayo kupitia huduma ya Mixx, Salum alieleza:
“Ukitumia Super App ya Mixx, mteja atatafuta Mini App ya Osaju Parking, ambapo mara baada ya kubonyeza App hiyo, ataingiza nambari ya gari ili kuona bili yake na kufanya malipo. Vinginevyo, anaweza kuingia moja kwa moja kwenye tovuti ya Osaju ambayo itamwelekeza namna ya kufanya malipo. Kwa wateja wenye simu ndogo, wanaweza kutumia huduma ya USSD au kupitia watoa huduma wa Osaju, ambapo mteja atajiwekea namba ya siri mwenyewe ili kulipia.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uhifadhi na Maendeleo ya Mji Mkongwe, Ali Said Bakar, alisema mfumo huo mpya ni katika kutekeleza kwa vitendo dhamira ya Serikali ya Awame ya Nane ambapo Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezitaka Taasisi za Umma kuongeza kasi ya matumizi ya KIDIGITALI katika kutoa huduma kwa wateja kwa lengo la kuimarisha ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.





“Kupitia mfumo huu wa kidigitali, tunapata suluhisho lenye uwazi, usalama na linalowarahisishia wananchi kufanya malipo kwa wakati wowote na mahali popote,” alisema Ali.
“Tunaamini ushirikiano huu na Mixx na Osaju utasaidia kuimarisha utendaji wa Mamlaka, kuongeza mapato na kuboresha mazingira ya utoaji huduma kwa wananchi wa Zanzibar,” aliongeza.
Kwa sasa, mfumo huo unatekelezwa katika maeneo yote yaliyo chini ya STCDA yakiwemo Darajani, Malindi, Forodhani, Vuga, Bandarini na maeneo mengine ya Mji Mkongwe.
Naye, Mkurugenzi wa Osaju Company Ltd, Farida Said Uledi, alisema:
“Tumejidhatiti kuhakikisha mfumo huu unakuwa wa mfano katika utoaji wa huduma za kidigitali nchini. Ushirikiano huu na Mixx na STCDA ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kutumia teknolojia kuboresha huduma za maegesho, kupunguza changamoto za malipo ya fedha taslimu na kuimarisha usimamizi wa maeneo ya kuegesha magari.”
“Kupitia mfumo huu, tumeweka msingi imara wa kubadilisha namna wananchi wanavyofanya miamala ya maegesho kwa uwazi na ufanisi zaidi. Tunaamini hii ni mwanzo wa mageuzi chanya katika ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma bora kwa wananchi wa Zanzibar,” aliongeza Farida.





