HomeHabariMmarekani wa miaka 90 aweka rekodi mpya Mlima Kilimanjaro

Mmarekani wa miaka 90 aweka rekodi mpya Mlima Kilimanjaro

Raia wa Marekani, Dk. Art Ulene, ameweka rekodi mpya kwa kufanikiwa kufika Kilele cha Uhuru cha Mlima Kilimanjaro akiwa na umri wa miaka 90, na kuwa mtu mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kufikia kilele cha mlima huo mrefu zaidi barani Afrika.

Dk. Ulene alianza safari yake ya kuupanda Mlima Kilimanjaro Julai 2, 2026 na kufanikiwa kufika Uhuru Peak Julai 13, siku aliyotimiza miaka 90 ya kuzaliwa.

Akiwa kileleni, alikata keki kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa, tukio lililoweka rekodi mpya na kuonyesha kuwa umri si kikwazo cha kutimiza ndoto.

Akizungumza Julai 16 baada ya kushuka mlimani, Dk. Ulene alisema safari hiyo ilikuwa zawadi ya kipekee ya kutimiza miaka 90 na ushahidi kwamba maandalizi mazuri, uvumilivu na kutokata tamaa vinaweza kumwezesha mtu kufikia malengo yake bila kujali umri.

“Ninafuraha sana kuupanda Mlima Kilimanjaro kusherehekea miaka yangu 90 ya kuzaliwa. Sasa narudi nyumbani nikiwa na ujumbe mmoja kwamba Tanzania ni nchi salama yenye watu wakarimu na vivutio vya kipekee. Nitakuwa balozi mzuri wa Tanzania na kuwahamasisha watu wengi zaidi kuja kuupanda mlima huu na kutembelea vivutio vingine,” alisema Dk. Ulene.

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (KINAPA), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Angela Nyaki, alisema mafanikio hayo yameandika historia mpya kwani rekodi ya awali ilikuwa ya raia mwingine wa Marekani aliyefika kileleni mwaka 2019 akiwa na umri wa miaka 89.

Alieleza kuwa kutokana na umri wa Dk. Ulene, KINAPA iliandaa mpango maalumu wa kuhakikisha anapanda mlima huo kwa usalama, ikiwemo kumpa zaidi ya siku 10 kukamilisha safari pamoja na mapumziko ya mara kwa mara ili kulinda afya yake.

“Tulihakikisha ndoto yake ya kufika kileleni inatimia bila kuhatarisha afya yake, na leo ameandika historia mpya. Mafanikio haya yanaonyesha kuwa kwa maandalizi sahihi na usimamizi wa kitaalamu, watu wa rika mbalimbali wanaweza kutimiza ndoto ya kuupanda Mlima Kilimanjaro,” alisema Nyaki.

Kwa upande wake, mmiliki wa kampuni ya utalii ya World Wide Trekking, Dean Cardinale, alisema rekodi hiyo ni chachu kwa sekta ya utalii kwani itaendelea kuitangaza Tanzania duniani na kuwahamasisha watu wa rika zote kutembelea na kuupanda Mlima Kilimanjaro, moja ya vivutio vikubwa vya utalii barani Afrika.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments