HomeAfyaWS4H yaacha urithi endelevu, serikali yapongeza mafanikio

WS4H yaacha urithi endelevu, serikali yapongeza mafanikio

Serikali imesema itatumia uzoefu na mafanikio yaliyopatikana kupitia Mradi wa Mifumo ya Maji, Usafi wa Mazingira na Afya (WS4H) kuboresha na kupanua huduma hizo nchini, ikieleza kuwa mradi huo umeweka msingi imara wa utoaji wa huduma endelevu zinazostahimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Morogoro na Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Maji, Diana Kimario, wakati wa hafla ya kuhitimisha mradi wa WS4H iliyowakutanisha zaidi ya washiriki 80 kutoka taasisi za Serikali, washirika wa maendeleo na mashirika ya kiraia kutathmini mafanikio na mafunzo yaliyopatikana katika utekelezaji wake.

Akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri, Kimario alisema mafanikio ya mradi huo yameonyesha kuwa uboreshaji wa huduma za maji, usafi wa mazingira na afya hauwezi kutegemea ujenzi wa miundombinu pekee, bali unahitaji pia taasisi imara, mifumo madhubuti na ushirikiano wa wadau ili kuhakikisha huduma zinakuwa endelevu.

Alisema Serikali itaendelea kuingiza mafunzo na uzoefu uliopatikana kupitia WS4H katika mipango mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji na Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya.

Kimario alisema athari za mabadiliko ya tabianchi zimeongeza umuhimu wa kuwa na mifumo ya maji, usafi wa mazingira na afya yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto hizo ili kulinda afya za wananchi, vituo vya kutolea huduma za afya na shughuli za uzalishaji.

Aidha, aliipongeza Taasisi ya Maendeleo ya Uholanzi (SNV) pamoja na Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo ya Uingereza (FCDO) kwa kufadhili na kuutekeleza mradi huo tangu mwaka 2024.

Alisema kupitia WS4H, uwezo wa taasisi umejengwa, wataalamu wameimarishwa, mifumo ya takwimu imeboreshwa na mipango ya maendeleo imeendelea kuandaliwa kwa kuzingatia ushahidi, hatua ambazo zimechangia kuimarisha huduma za maji vijijini.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Sekta ya Maji wa SNV Tanzania, Olivier Germain, alisema ingawa utekelezaji wa WS4H umefikia tamati, maarifa, ushirikiano na mafanikio yaliyopatikana yataendelea kuwa nguzo muhimu katika safari ya Tanzania ya kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma salama, za uhakika na endelevu za maji, usafi wa mazingira na afya.

“Mradi unahitimishwa, lakini maarifa, ushirikiano na mafanikio yaliyopatikana yataendelea kuimarisha safari ya Tanzania kuelekea huduma endelevu za maji, usafi wa mazingira na afya kwa wote,” alisema Germain.

Mradi wa WS4H, unaotekelezwa na SNV kwa ufadhili wa FCDO, ulitekelezwa katika mikoa ya Dodoma, Arusha na Simiyu ukilenga kuboresha upatikanaji wa huduma salama za maji, usafi wa mazingira na afya, pamoja na kuimarisha mipango, uratibu na mifumo inayostahimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kupitia ushirikiano kati ya Wizara ya Maji, Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais–TAMISEMI na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), mradi huo umechangia kuimarika kwa huduma za maji na usafi wa mazingira, pamoja na kuongeza uwezo wa taasisi na wadau kutoa huduma jumuishi na endelevu kwa wananchi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments