Mwanahabari na mchambuzi wa masuala ya kimataifa, Kelvin Raphael maarufu Zungu, amesema bei za mafuta nchini Tanzania zinaendelea kuwa nafuu kuliko katika nchi nyingi zinazoizunguka, zikiwemo zenye bandari na zisizo na bandari, ambapo lita moja ya petroli katika Jiji la Dar es Salaam inauzwa kwa Sh3,990, ikilinganishwa na Sh4,230 nchini Msumbiji, Sh4,336 nchini Kenya, Sh4,520 Afrika Kusini, zaidi ya Sh5,400 nchini Rwanda na takribani Sh10,000 kwa lita nchini Malawi, licha ya mvutano unaoendelea Mashariki ya Kati unaoendelea kutishia soko la mafuta duniani.
Zungu alisema tofauti hiyo inaonyesha kuwa Tanzania imeendelea kunufaika na mfumo wa Bulk Procurement System (BPS) unaowezesha ununuzi wa pamoja wa mafuta kwa ushindani wa zabuni, pamoja na ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam na usimamizi wa bei unaofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Alisema hatua hizo zimeifanya Tanzania kuendelea kuwa na ushindani mkubwa wa bei za mafuta ukilinganisha na nchi nyingi za Afrika Mashariki na Kusini.
Alisema soko la mafuta duniani linaendelea kuwa katika tahadhari kutokana na mvutano wa Mashariki ya Kati, hususan katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, ambako hupitia takribani asilimia 20 ya mafuta yanayouzwa duniani.
Hali hiyo imeongeza gharama za bima na usafirishaji wa mafuta, huku bei ya mafuta ghafi ikiendelea kuwa na mabadiliko kutokana na hofu ya kuvurugika kwa mnyororo wa usambazaji.
Kwa mujibu wa Zungu, Tanzania inaagiza mafuta yaliyokwisha kusafishwa kutoka Falme za Kiarabu (UAE), Saudi Arabia, Oman na Kuwait, hivyo changamoto yoyote ya kiusalama katika Mlango wa Hormuz inaweza kuongeza gharama za usafirishaji na kuathiri bei za mafuta katika masoko mengi duniani, ikiwemo Tanzania.
Hata hivyo, alisema uwezo wa Tanzania kuendelea kuwa na mafuta ya bei nafuu unaonyesha uimara wa sera za usimamizi wa sekta ya mafuta, uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam na mfumo wa ununuzi wa pamoja, ambao umeendelea kupunguza gharama za uagizaji wa mafuta na kuongeza ushindani wa soko.
Zungu ameishauri Serikali kuendelea kuimarisha uwezo wa taifa wa kuhifadhi mafuta ya akiba ili kulinda uchumi dhidi ya mishtuko ya soko la dunia na kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea hata endapo kutatokea changamoto katika usafirishaji wa mafuta kutoka Mashariki ya Kati.




