HomeHabariTaTEDO-SESO yapata ruzuku ya Sh bilioni 8 kukuza nishati safi

TaTEDO-SESO yapata ruzuku ya Sh bilioni 8 kukuza nishati safi

Taasisi ya TaTEDO–Sustainable Energy Services Organization (TaTEDO-SESO) na Ubalozi wa nchi ya Kifalme ya Norway nchini Tanzania zimesaini mkataba wa ruzuku wenye thamani ya hadi Krona za Norway (NOK) milioni 30, sawa na takribani Sh bilioni 8, kwa ajili ya kutekeleza programu ya miaka mitatu ya Mpito wa Nishati nchini.

Programu hiyo inalenga kuharakisha upatikanaji wa suluhisho za upishi safi na matumizi ya nishati endelevu, sambamba na kuchochea maendeleo ya sekta ya nishati nchini kwa manufaa ya wananchi.

Makubaliano hayo yanaendeleza ushirikiano wa muda mrefu kati ya Serikali ya Norway na TaTEDO-SESO katika kusaidia juhudi za Tanzania za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha maendeleo endelevu na kukuza uchumi shirikishi kupitia huduma za kisasa za nishati.

Mpango huo utaenda sambamba na utekelezaji wa Mission 300 Energy Compact pamoja na Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034 unaolenga kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa za kupikia na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.

Mission 300 ni mpango mkubwa wa pamoja ulioanzishwa na Benki ya Dunia (World Bank) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) wenye lengo la kuiunganisha jamii ya watu milioni 300 barani Afrika kwenye umeme ifikapo mwaka 2030.

Kupitia programu hiyo, inatarajiwa kuongeza matumizi ya teknolojia za upishi safi, kupanua matumizi ya nishati jadidifu kwa kaya, taasisi na shughuli za uzalishaji, pamoja na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji wa nishati safi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utiaji saini, Balozi wa Norway nchini Tanzania alisema serikali yake itaendelea kuunga mkono ajenda ya maendeleo endelevu ya Tanzania kupitia miradi yenye matokeo yanayopimika katika upatikanaji wa nishati safi na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TaTEDO-SESO, Mhandisi Estomih  Sawe, aliishukuru Serikali ya Norway kwa kuendelea kuiamini taasisi hiyo na kuunga mkono juhudi zake za kuendeleza nishati safi nchini.

Alisema ruzuku hiyo ni uwekezaji wa kimkakati utakaowezesha utekelezaji wa malengo ya Mission 300 na Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwa kupanua upatikanaji wa huduma za kisasa za nishati na kuimarisha soko la upishi safi.

Mhandisi Sawe alisema matumizi ya nishati safi yatasaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kuhifadhi misitu, kuboresha afya ya wananchi kwa kupunguza uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba na kuongeza ajira za kijani kwa wanawake na vijana.

Alisisitiza kuwa mafanikio ya programu hiyo yatategemea ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, taasisi za fedha, taasisi za utafiti, asasi za kiraia na wananchi pamoja na kuwepo kwa mazingira rafiki ya uwekezaji.

TaTEDO-SESO imeahidi kutekeleza programu hiyo kwa kuzingatia uwazi, uwajibikaji, weledi na kuhakikisha fedha zote zinazowekezwa zinaleta matokeo yenye manufaa ya muda mrefu kwa wananchi.

Mradi huo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za kisasa za nishati, kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi, kuboresha afya ya jamii na kuongeza uwekezaji pamoja na ajira za kijani nchini.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments