HomeHabariWatu sita wahukumiwa kunyongwa hadi kufa, wanne wakamatwa na silaha Tabora

Watu sita wahukumiwa kunyongwa hadi kufa, wanne wakamatwa na silaha Tabora

Mapambano dhidi ya uhalifu mkubwa mkoani Tabora yamechukua sura mpya baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kuwahukumu watu sita kunyongwa hadi kufa kwa makosa ya mauaji, huku Jeshi la Polisi likisema hukumu hizo zinaakisi mafanikio ya uchunguzi na usimamizi wa kesi za jinai.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Twaha Lulengelule, alisema Julai 17, 2026 kuwa hukumu hizo ni sehemu ya mafanikio yaliyopatikana katika kesi zilizokuwa zikisikilizwa mahakamani pamoja na operesheni mbalimbali zilizotekelezwa na jeshi hilo kuanzia Juni hadi Julai mwaka huu.

Alisema Julai 13, 2026, Mahakama Kuu Kanda ya Tabora iliwatia hatiani Majuto Lutema (32), Sida Mayeka (47), Kulwa Masunga Senga (44) na Iddy Ramadhani (35), wote wakazi wa Wilaya ya Sikonge, na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kosa la mauaji.

Lulengelule alisema pia Mussa Marko (28), mkazi wa Ushirombo wilayani Kahama, alihukumiwa kunyongwa hadi kufa Juni 19, 2026, huku Chandika Fideli (36), mkazi wa Kijiji cha Mkola wilayani Urambo, naye akihukumiwa adhabu hiyo Juni 17, 2026 baada ya kutiwa hatiani kwa kosa hilo.

Mbali na mafanikio ya kesi za mauaji, Kamanda Lulengelule alisema operesheni na doria zilizofanyika Julai 18, 2026 katika Pori la Nkomango, Kata ya Kiwele wilayani Sikonge, ziliwezesha kukamatwa kwa watuhumiwa wanne waliokuwa wakimiliki bunduki aina ya Rifle Model 70-458 isiyo na namba pamoja na risasi tatu bila kibali. Alisema watuhumiwa hao tayari wamefikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.

Aidha, alisema operesheni nyingine zilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa tisa waliokutwa na dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilogramu 117 pamoja na kete 2,062 katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tabora. Watuhumiwa wote wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Katika kipindi hicho, Jeshi la Polisi pia lilikamata jumla ya makosa 9,109 ya usalama barabarani na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika, huku likiendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara ili kuongeza uzingatiaji wa sheria na kupunguza ajali.

Kamanda Lulengelule aliwataka wananchi kuachana na vitendo vya uhalifu na kujihusisha na shughuli halali za kujipatia kipato, akionya kuwa Jeshi la Polisi halitasita kuwachukulia hatua kali wote watakaojihusisha na mauaji, biashara ya dawa za kulevya, umiliki haramu wa silaha, ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani na vitendo vingine vinavyokiuka sheria za nchi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments