DAR ES SALAAM: Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimeandaa kongamano la kisayansi linalolenga kujadili matokeo ya tafiti kuhusu usugu wa vimelea dhidi ya dawa kwa binadamu na wanyama, pamoja na kuhamasisha ufugaji wa kisasa unaozingatia usafi wa mazingira ili kupunguza maambukizi yanayochochea usugu huo.
Akifungua kongamano hilo jijini Dar es Salaam Juni 3, 2026, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Maalum ya Kitaifa ya Kupambana na Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa, Profesa Hezron Nonga, amesema juhudi zinazofanywa na Serikali, taasisi za elimu na wadau wa afya zimechangia kupungua kwa vifo vinavyohusishwa na usugu wa vimelea dhidi ya dawa.
Amesema jamii inapaswa kuendelea kupewa elimu kuhusu athari za usugu wa vimelea katika afya ya binadamu na mifugo, huku akibainisha kuwa matumizi holela ya dawa za antibiotiki yamepungua kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.


Kwa mujibu wa Profesa Nonga, ambaye pia ni mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), matumizi sahihi ya dawa yamechangia kudhibiti ongezeko la usugu wa vimelea, ingawa changamoto hiyo bado inaendelea kuwa tishio kwa afya ya umma.
“Usugu wa vimelea dhidi ya dawa bado upo na unaendelea kuongezeka. Ndiyo maana Serikali iliunda kamati maalum ya kitaifa ili kuratibu juhudi za kukabiliana na changamoto hiyo,” amesema Profesa Nonga.
Ameongeza kuwa ushiriki wa vyuo vikuu, taasisi za utafiti na sekta binafsi unaimarisha mapambano dhidi ya tatizo hilo kwa kusaidia uzalishaji wa maarifa mapya na mbinu bora za kukabiliana nalo.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa MUHAS anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Profesa Erasto Mbugi, amesema chuo hicho kina jukumu muhimu la kufundisha, kufanya tafiti na kutoa huduma za afya, hivyo kina mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya usugu wa vimelea.
Amesema kongamano hilo limebeba agenda muhimu ya kuwajengea wanafunzi na wataalamu wa afya uelewa wa kina kuhusu athari za usugu wa vimelea, hususan katika matibabu ya magonjwa ya kuambukiza.
Profesa Mbugi amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuandaa mafunzo na warsha kwa wataalamu wa afya ili kuongeza uelewa kuhusu matumizi sahihi ya dawa, sambamba na kuimarisha tafiti zitakazosaidia kubuni mbinu mpya za matibabu na dawa zenye uwezo wa kukabiliana na vimelea sugu.



Amesema kongamano hilo pia linatoa fursa kwa watafiti, wanafunzi na watoa huduma za afya kubadilishana uzoefu, kujifunza matokeo ya tafiti mbalimbali na kujenga uwezo wa pamoja katika kudhibiti tatizo hilo.
Naye mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili ya Microbiology katika MUHAS, Lilian Kiwone, amesema kongamano hilo limewapa wanafunzi nafasi ya kuelewa kwa undani ukubwa wa changamoto ya usugu wa vimelea na wajibu wa wanasayansi katika kutafuta suluhisho la kudumu.
Amesema maarifa yanayotolewa kupitia tafiti zinazowasilishwa yatawawezesha wanafunzi kufanya tafiti zenye tija, kuelimisha jamii na kushiriki kikamilifu katika juhudi za kupunguza kasi ya kuenea kwa usugu wa vimelea dhidi ya dawa.
“Tumepata uelewa mpana zaidi kuhusu namna ambavyo sisi kama wanafunzi na watafiti wa baadaye tunaweza kushiriki katika kuisaidia jamii kudhibiti usugu wa vimelea dhidi ya dawa,” amesema Kiwone.





