Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA),imetoa mafunzo Kwa vijana 878 kwa ajili ya kuwajengea uwezo ili kufahamu haki zao katika Zabuni zinazotolewa na serikali.
Aidha,inatarajia kuunganisha Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) na mfumo wa Mahakama ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za rufaa.
Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando amesema hatua ya kuunganisha mifumo hiyo inatarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka wa fedha ujao ikiwa ni sehemu ya kuimarisha matumizi ya teknolojia na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.
Amesema matumizi ya mfumo wa NeST yameendelea kurahisisha uwasilishaji wa malalamiko na rufaa, kuhifadhi kumbukumbu pamoja na kuongeza uwazi katika kushughulikia mashauri ya zabuni za umma.

“Matumizi ya mfumo huo yamerahisisha utunzaji wa kumbukumbu, kuongeza uwazi katika kushughulikia rufaa na kumwezesha mzabuni kufuatilia hatua iliyofikiwa kwenye shauri lake akiwa popote,” amesema.
Sando amesema PPAA imeendelea kutoa mafunzo katika kanda mbalimbali nchini ili kuongeza uelewa wa wadau wa ununuzi wa umma, ambapo wazabuni 1,296 pamoja na watumishi wa idara za ununuzi na sheria 705 wamepatiwa elimu kuhusu matumizi ya mfumo wa kushughulikia malalamiko na rufaa.
Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwasaidia washiriki kutambua fursa zilizopo katika zabuni za Serikali, kuelewa haki zao na kushiriki kikamilifu katika michakato ya ununuzi wa umma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema vijana, wanawake na makundi maalum wanapaswa kutumia mafunzo hayo kuongeza ushiriki wao katika zabuni za Serikali na kujinufaisha kiuchumi.
Amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa makundi mbalimbali kushiriki katika ununuzi wa umma, huku akisisitiza matumizi ya mifumo ya kidijitali yanaweza kuongeza uwazi na kupunguza ucheleweshaji wa taarifa.






