Mashirika wanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) yamesema watu 1,605 wameuawa nchini kutokana na migogoro ya kimahusiano katika kipindi cha mwaka 2024 hadi Juni 2026, huku wanawake wakitajwa kuwa miongoni mwa waathirika wakubwa wa mauaji hayo.
Kwa mujibu wa waraka uliotolewa na wanachama wa mtandao huo Oktoba 22, 2026, takwimu za Jeshi la Polisi zinaonesha kuwa matukio 941 ya mauaji yaliripotiwa kuanzia Januari hadi Juni 2026, ikilinganishwa na matukio 926 katika kipindi kama hicho mwaka 2025.
Waraka huo unaeleza kuwa kati ya matukio 941 ya mauaji yaliyoripotiwa katika nusu ya kwanza ya mwaka 2026, matukio 458 yalihusishwa na migogoro ya kimahusiano.
Aidha, mwaka 2024 yaliripotiwa matukio 2,193 ya mauaji, ambapo 422 yalihusishwa na migogoro ya kimahusiano, huku mwaka 2025 yakiripotiwa matukio 1,977 ya mauaji, yakiwemo 725 yaliyotokana na migogoro hiyo.
THRDC imesema mauaji hayo yanachochewa na sababu mbalimbali, zikiwemo wivu wa kimapenzi, migogoro ya ndoa na familia, madai ya usaliti, tofauti za kifedha na changamoto za malezi ya watoto.
Katika waraka huo, mtandao huo umetaja matukio mbalimbali ya mauaji yaliyoripotiwa kati ya Julai na Oktoba 2026, yakiwemo mauaji ya Leah Mazengo wa Bahi, Dodoma, na Margeth Hamis Richard wa Musoma, mkoani Mara, pamoja na matukio mengine yaliyohusisha wanawake na watoto katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, umeeleza kuwa baadhi ya watoto wamekuwa waathirika wa moja kwa moja wa migogoro ya kimahusiano, ikiwemo kushambuliwa na kuuawa. Miongoni mwa matukio yaliyotajwa ni la watoto wawili, msichana wa miaka minane na mvulana wa miaka 10, waliouawa na baba yao mkoani Morogoro kabla ya baba huyo kujiua.
Mtandao huo umesema ongezeko la matukio hayo linachangiwa pia na udhaifu wa mifumo ya kuzuia ukatili, ukosefu wa elimu kuhusu mahusiano salama, changamoto za afya ya akili, pamoja na upungufu wa wataalamu wa ustawi wa jamii na huduma za ushauri nasaha.
Kwa mujibu wa waraka huo, baadhi ya mauaji hutokea baada ya viashiria vya ukatili kuwapo kwa muda mrefu, vikiwemo vitisho vya kuua, vipigo vya mara kwa mara, udhibiti wa mwenza na unyanyasaji wa kisaikolojia.
Kutokana na hali hiyo, THRDC imeitaka Serikali kuimarisha mifumo ya kupokea na kufuatilia taarifa za vitisho, kuongeza Maafisa Ustawi wa Jamii na kuweka mifumo madhubuti ya kuwalinda watu walio katika hatari ya kufanyiwa ukatili.
Pia, mtandao huo umelitaka Bunge kutunga sheria mahsusi ya kuzuia ukatili wa kijinsia na ukatili wa majumbani, huku ukiziomba taasisi za elimu, viongozi wa dini, vyombo vya habari na jamii kwa ujumla kuimarisha elimu kuhusu utatuzi wa migogoro kwa njia za amani.
Katika kuendeleza mapambano dhidi ya mauaji hayo, THRDC na mashirika mengine ya utetezi wa haki za binadamu yametangaza kuanzisha kampeni endelevu yenye kauli mbiu “Mapenzi Siyo Vita; USIUE”, kwa lengo la kuhamasisha jamii kukataa ukatili na kuheshimu haki ya kila mtu kuishi na kufanya maamuzi kuhusu mahusiano yake.
Mtandao huo umesisitiza kuwa hakuna sababu ya kimapenzi inayoweza kuhalalisha mauaji, ukieleza kuwa mahusiano yanaposhindikana, wahusika wanapaswa kutafuta suluhisho la amani au kuachana bila kutumia vitendo vya ukatili.




