HomeHabariOSHA yaweka mwelekeo mpya wa utendaji

OSHA yaweka mwelekeo mpya wa utendaji

Ofisi ya Msajili wa Hazina imesema Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ni miongoni mwa Taasisi muhimu kwa maendeleo ya Tanzania kutokana na jukumu lake la msingi la kusimamia masuala ya usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Usimamizi Rasilimali Watu katika Taasisi za Umma-Ofisi ya Msajili wa Hazina, Hussein Kakurwa, katika mafunzo elekezi kuhusu majukumu ya Bodi ya Ushauri ya OSHA yaliyofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, Kibaha Mkoani Pwani.

“Kama tunavyojua suala la usalama na afya ni la msingi sana na ili Taifa lolote liweze kuendelea ni lazima lihakikishe watu wake wanafanya kazi katika mazingira salama na wanakuwa na afya njema. Kwahiyo jukumu ambalo OSHA wamepewa ni la msingi sana na Ofisi ya Msajili wa Hazina tunaichukulia OSHA kuwa miongoni mwa Taasisi nyeti na za kimkakati katika jukumu la serikali ya kusukuma maendeleo ya wananchi, ameeleza Kakurwa.

Aidha, amesema Ofisi ya Msajili wa Hazina inajukumu la kuendesha mafunzo kwa viongozi wa Taasisi za umma ili kuwafahamisha na kuwakumbusha kuhusu majukumu yao ya msingi kwa mujibu wa sheria zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Mwenyekiti wa Bodi ya OSHA Makwaia Makani amewahakikishia wafanyakazi nchini kuwa Bodi yake itakuwa karibu na waajiri wote ili kuhakikisha kwamba wanaboresha mazingira ya kazi ili kulinda afya, usalama na ustawi wa wafanyakzi.

Ameongeza kuwa mafunzo elekezi waliyoyapata yamewapa fursa ya kuielewa kikamilifu Taasisi ya OSHA nahivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kusimamia na kufuatilia utendaji wa Taasisi hiyo. 

Mjumbe wa Bodi hiyo, Rehema Ludanga, amesema baada ya mafunzo hayo ni wajibu wao kama Bodi kutumia maarifa na uzoefu wao katika kumshauri Waziri na Menejimenti ya OSHA ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya msingi ya Taasisi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda ambaye kwa mujibu wa muundo ndiye Katibu wa Bodi hiyo, amewashukuru viongozi wa juu kwa kuhakikisha Taasisi ya OSHA inapata Bodi mpya baada ya iliyokuwepo kuhitimisha kipindi chake.

“Tumekuwa na mafunzo mazuri sana ambapo wajumbe wamepitishwa katika sheria, mpango mkakati wa Taasisi na masuala mengine muhimu yanayohusu utendaji wa Taasisi yatu. Tunamshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri wetu, Mheshimiwa Deus Sangu kwakuona umuhimu wa kuunda Bodi ili iweze kuishauri serikali kuhusiana na utendaji wa Taasisi hii,” amesema Mtendaji Mkuu na kuongeza:

“Nasisi tumeiahidi Bodi kwamba malengo yote tuliyoyaweka katika mpango mkakati wetu wa miaka mitano (2026-2031) ambayo yamezingatia vipaumbele vya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 tutayatekeleza ipasavyo.”

Bodi ya Ushauri ya OSHA iliundwa hivi karibuni na kuzinduliwa rasmi Mei 25, 2026 Jijini Dar es Salaam ambapo miongoni mwa majukumu ya msingi ya Bodi hiyo ni kumshauri Waziri mwenye Dhamana ya Masuala ya Kazi, Ajira na Mahusiano kuhusiana na utendaji wa Taasisi ya OSHA hususan katika kuandaa vipaumbele, mipango na bajeti pamoja na kufuatilia utekelezaji wa mipango hiyo ili kufikia malengo ya Taasisi. 

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments