HomeBiasharaKitabu muongozo matumizi salama gesi ya kupikia chazinduliwa

Kitabu muongozo matumizi salama gesi ya kupikia chazinduliwa

Katika kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha wananchi wanaondokana na matumizi ya majiko ya mkaa, wadau wa nishati safi wamezindua kitabu maalum cha mwongozo wa matumizi salama ya gesi ya kupikia (LPG).


‎Uzinduzi wa kitabu hicho umefanyika jana jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ushirikiano wa kutoa mafunzo ya matumzi ya nishati ya kupikia kati ya Chama cha Skauti Tanzania na kampuni ya Oryx Gas Tanzania.


‎Kitabu hicho ambacho kitasambazwa mashuleni, majumbani na kwenye taasisi mbalimbali kina lenga kutoa elimu ya matumizi sahihi ya gesi ya kupikia ili kuepuka majanga ya moto yanayotokana na kulipuka kwa mtungi wa gesi.




‎Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho na utiaji saini wa makubaliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Gas Tanzania, Benoit Araman alisema hiyo yote ni kuunga mkono juhudi za serikali kuona watanzania wote wanatumia nishati hiyo kweye kupikia.


‎Alisema pamoja na kuwa kampuni ina wajibu kwa wanahisa, wafanyakazi na serikali, bado wanamini wananchi ndio wadau wake wakuu, hivyo imeamua kuwekeza katika elimu ya usalama ili kupunguza ajali zinazotokana na matumizi yasiyo sahihi ya gesi.


‎”Tunataka kuona Watanzania wengi zaidi wakitumia gesi ya LPG kwa usalama, ni wazi hatuwezi kuwafikia mamilioni ya watumiaji peke yetu, ndiyo maana tumeamua kushirikiana na Chama cha Skauti Tanzania ambacho kina mtandao mkubwa wa vijana wanaoweza kuifikisha elimu hii kwa jamii na kufikia malengo” alisema.


‎Alieleza kuwa kupitia makubaliano hayo, Kampuji hiyo itawajengea uwezo wakufunzi wa Skauti ambao baadaye watawafundisha wananchi katika maeneo mbalimbali nchini kwa kutumia mbinu ya kumfundisha mkufunzi ili naye awafundishe wengine.


‎Araman alisema kitabu hicho kimeandaliwa kwa ushirikiano na Meneja wa Mafunzo wa Oryx Gas, Peter Ndomba pamoja na vyanzo kutoka chama cha wazalishaji gesi ya kupiki duniani  kikilenga kuwa rejea ya kudumu kwa watumiaji wa gesi ya LPG.


‎”Ni muhimu kuwa na nyenzo ambayo mtu anaweza kuishika mkononi, akaisoma mara kwa mara na kuirejea kila anapohitaji kujifunza matumizi salama ya gesi,” alisema.




‎Akielezea zaidi uzinduzi wa kitabu hicho, alisema kitapatikana katika nakala za kuchapishwa pamoja na mfumo wa kidijitali ili kuwafikia wananchi wengi zaidi nchini.


‎”Tunahakikisha kila anayechagua kutumia gesi anakuwa salama. Kitabu hiki kitampa mtumiaji uelewa mpana wa matumizi salama ya gesi ya LPG na kitatumika pia kufundishia katika taasisi mbalimbali ikiwemo shule mara baada ya kukamilisha taratibu za kupata hatimiliki,” alisema.


‎Kwa upande wake, Skauti Mkuu wa Tanzania, Rashid Mchatta, alisema tukio hilo si la kusaini makubaliano pekee na kuzindua kitabu, bali ni mwanzo wa safari ya kuwajengea vijana maarifa, ujuzi na fursa zitakazochangia maendeleo ya taifa.


‎Alisema Skauti inaamini kuwa kijana mwenye maarifa, maadili na nidhamu ni nguvu muhimu kwa maendeleo ya Tanzania, hivyo ushirikiano huo utasaidia kuwajengea vijana uwezo katika matumizi ya nishati safi, ajira na usalama.


‎”Tutahakikisha ushirikiano huu unatekelezwa kwa umakini ili vijana wetu wawe mabalozi wa elimu ya matumizi salama ya gesi na kusaidia kupunguza ajali zinazotokana na matumizi yasiyo sahihi ya LPG kupitia mwongozo wa kitabu hiki kilichozinduliwa leo ( jana).


‎Aidha, Kamishna  Mkuu wa Skauti, Abubakar Mtitu, alisema ushirikiano huo unaendana na misingi ya Skauti ya kuitumikia jamii na kuwajengea vijana uwezo wa kushiriki katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.


‎Alisema Skauti itaendelea kutumia mtandao wake wa vijana kueneza elimu ya matumizi salama ya gesi pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ili kuchangia ustawi wa jamii na mazingira.


RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments