Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Sera, Mahusiano ya Serikali na Ushirikiano kwa Afrika wa Gates Foundation, Caty Fall Sow, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika afya ya mama na mtoto nchini na barani Afrika.
Mazungumzo hayo yalifanyika Ikulu, Dar es Salaam, wakati Rais Samia akiendelea kutekeleza jukumu lake kama Kinara wa Afya ya Mama na Mtoto barani Afrika, likilenga kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu, wawili hao walijadili ushirikiano katika chanjo, lishe, kudhibiti magonjwa na kuimarisha mifumo ya huduma za afya kwa wananchi.
Caty Fall Sow, amempongeza Rais Samia kwa kuteuliwa kuwa kinara wa Afya ya Mama na Mtoto, akisema nafasi hiyo itasaidia kuhamasisha nchi za Afrika kuongeza juhudi za kuboresha afya ya wanawake, watoto na watoto wachanga kupitia uwekezaji endelevu.
Rais Samia, amesema Tanzania imeendelea kuimarisha miundombinu na huduma za afya ya uzazi. Pia alieleza maandalizi ya ramani ya Afrika itakayohamasisha uwajibikaji, uwekezaji na utekelezaji wa mikakati ya kuokoa maisha ya mama na mtoto.





