Takriban siku 16 za Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, banda la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) limewahudumia wageni 1,600, Meneja wa PSSSF Kanda ya Ilala Amina Kassim amesema.
Amesema wageni hao waliojumuisha viongozi wa Serikali, wananchi, wanachama na wastaafu wanaopokea pensheni PSSSF, walipata elimu kuhusu hifadhi ya jamii, huku wanachama na wastaafu wakielekezwa namna ya kutumia huduma za kidijitali kupitia PSSSF Kiganjani na PSSSF Member Portal, alibainisha.
“Kupitia mifumo hiyo, wanachama waliwezeshwa kufuatilia taarifa za mafao, kuwasilisha madai, kuhuisha taarifa za wategemezi, kuuliza maswali na kupata taarifa mbalimbali za Mfuko, ikiwemo uwekezaji, kwa urahisi kupitia simu janja.” Alisisitiza Kassim.


Aidha, wananchi walipata fursa ya kufahamu kwa kina uwekezaji wa PSSSF katika Kiwanda cha Bidhaa za Ngozi (KLICL), Machinjio ya Kisasa ya Nguru Hills, majengo ya biashara na makazi, pamoja na viwanja vinavyomilikiwa na Mfuko, alisema.
Alisema, Maonesho haya yamekuwa jukwaa muhimu la kuonesha mchango wa uwekezaji wa PSSSF katika maendeleo ya taifa. Kupitia banda la Mfuko, wananchi walipata fursa ya kununua nyumba kwa malipo ya papo hapo au kwa utaratibu wa ahadi, kununua bidhaa bora za ngozi zinazozalishwa na KLICL, kama vile viatu, mikoba na mikanda, pamoja na nyama yenye ubora wa kimataifa kutoka Machinjio ya Nguru Hills.
“Uwekezaji huu unaonesha dhamira ya PSSSF ya kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza uzalishaji, ajira na kuendelea kutoa manufaa ya moja kwa moja kwa wanachama wake na Watanzania kwa ujumla,” alifafanua na kuhitimisha kwa kusema. “Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, tunatoa shukrani za dhati kwa wananchi wote, wanachama, waajiri, wadau na wageni wote waliotembelea banda letu na kushiriki nasi katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.






