Tuesday, February 17, 2026
spot_img
HomeBiasharaTRA yasisitiza matumizi ya mfumo wa IDRAS

TRA yasisitiza matumizi ya mfumo wa IDRAS

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda amewaonya wafanyabiashara wanaodanganywa na madalali kuwa watawafutia madeni ya kodi na kuwataka kufika kwenye ofisi za mamlaka hiyo kama wanachangamoto.

Kamishna Mwenda amesema kwa kawaida deni la kodi halifutiki mpaka mhusika anapoamua kulilipa au kulipinga na kushinda kesi mahakamani.

Aliyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizindua Kituo cha Huduma kwa Wateja eneo la Masaki Kinondoni jijini Dar es Salaam, kituo ambacho kinatarajiwa kuwahudumia zaidi ya walipa kodi 6,000.

Amesema kuna baadhi ya wafanyabiashara wenye madeni ambao wanadhani kuwa wanaweza kufanya mchezo kwa kuwatumia watu wa mitaani na  madeni yakafutika hali aliyoielezea kuwa ni kujidanganya na kupoteza muda wao.

“Nataka niwaambie wafanyabiashara tena wa nchi nzima kuwa kodi haifutiki isipokuwa kwa mambo mawili tu, aidha umeilipa au umeipinga ukaenda mahakamani na mahakama ikasema vinginevyo lakini nje ya hapo utadanganywa tukikugundua utalipa gharama mara mbili utalipa kodi yenyewe na faini,” amesema

Amesema mfanyabiashara yeyote mwenye changamoto ya kikodi anapaswwa kufika kwenye mamlaka hiyo kupata ushauri kwa wahusika badala ya kuhangaika na watu wa mitaani wasiokuwa na ujuzi wa kodi.

Amesema wafanyabiashara pia wanaweza kuwatumia washauri wa kodi ambao wamesajiliwa kisheria kufanya kazi hiyo badala ya kutafuta njia za mkato mkato kwa watu wa mitaani.

“Unaweza kupata ugonjwa wa moyo kwa kudanganywa, ukiwa na deni la kodi dawa ni moja tu kulilipa kwa wakati na kwa usahihi, kodi ikisimamiwa vizuri kunakuwa na usawa, mwenye kipato kidogo wanalipa kidogo na wenye kipato kikubwa walipe kikubwa,” amesema Mwenda

Aidha, amesema kuna baadhi ya wafanyabiashara wanaamini kuwa wafanyabiashara wakubwa hawalipi kodi wanayostahili kama wale wadogo.

Hivyo amesema  kuanzishwa kwa kituo cha huduma kwa wateja Masaki ni uthibitisho wa kutosha kuwa hata wafanyabaishara wakubwa wanalipa kodi kama walipakodi wengine.

Kamishna amesema wanatarajia mamlaka hiyo itakuwa na vituo kama hivyo 71 nchi nzima ili iwe rahisi kuwafikia wateja wake wa aina zote kuwarahishia ulipaji kodi kwa hiyari kwa kuwapa elimu.

Pia Kamishna Mwenda amewataka wafanyabiashara kuendelea kutumia mfumo wa IDRAS kwani mfanyabiashara halazimiki kwenda ofisi za TRA kupata huduma za kikodi badala yake anatumia mfumo huo kufanya shughuli zake zote mwenyewe akiwa ofisini kwake.

Amesema mfumo huo unapatikana saa 24 na mteja anaweza kujihudumia mwenyewe kwa kuomba marejesho ya kodi kwa kutumia mfumo au kuomba msamaha wa kodi kwa kutumia mfumo.

“Unaweza kuandika barua au kuomba ufafanuzi wowote, ni mfumo ambao umekuja kuleta mabadiliko makubwa sana ya usimamizi wa kodi nchini, hivyo kama unachangamoto ya mfumo wa IDRAS watumishi wetu wako nchi nzima nenda ukahudumiwe,” amesema

Amewapongeza walipa kodi wa mkoa wa Kinondoni kwa namna ambavyo wanalipa kodi kwa hiyari hali ambayo imeuwezesha mkoa huo kufanya vizuri sana kwenye ukusanyaji wa mapato.

“Pia nawapongeza watumishi wa mamlaka kwa kutoa huduma nzuri ambazo zimewawezesha biashara zenu ziendelee kukua na nawahakikishia watumishi watakaokuwa kwenye kituo hiki wana weledi wa kutosha watawasadia,” amesema

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments