HomeAfyaTanzania yaeleza mafanikio ujumuishwaji watu wenye ulemavu COSP19

Tanzania yaeleza mafanikio ujumuishwaji watu wenye ulemavu COSP19


New York.
 Serikali ya Tanzania imesema imepiga hatua kubwa katika kuimarisha ustawi na ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu, huku ikisisitiza umuhimu wa kuongeza upatikanaji wa vifaa na teknolojia saidizi ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.

Akihitimisha ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 19 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (COSP19-CRPD) uliofanyika New York, Marekani, Juni 11, 2026, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, alisema teknolojia na vifaa saidizi ni nyenzo muhimu katika kuwawezesha watu wenye ulemavu kuishi kwa kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika maendeleo.

“Ni muhimu kuendelea kuongeza upatikanaji na matumizi ya vifaa na teknolojia saidizi kwa watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi kwa usawa. Serikali inaendelea kutekeleza kwa vitendo dhana ya ujumuishwaji kwa kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata fursa na haki kwa usawa katika sekta mbalimbali,” alisema Mahundi.

Akizungumza kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Naibu Katibu Mkuu, Dk. James Kilabuko, alisema ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo umeiwezesha nchi kujifunza uzoefu na mbinu mbalimbali za kuboresha utekelezaji wa sera na programu za watu wenye ulemavu.

Alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika uwezeshaji na ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu, na kwamba kupitia mkutano huo imepata mbinu mpya zitakazosaidia kuimarisha juhudi hizo. Aidha, alibainisha kuwa Serikali itaandaa mpango kazi mahsusi kwa kushirikiana na wizara, taasisi na wadau mbalimbali ili kuimarisha utekelezaji na kushughulikia changamoto zilizobainishwa.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Maghembe, alisema Tanzania imeendelea kuboresha huduma za afya ya msingi kwa watu wenye ulemavu kwa kusogeza huduma karibu na wananchi, kuboresha miundombinu ya afya na kuwajengea uwezo watumishi wa sekta hiyo ili kutoa huduma jumuishi.

Aidha, alishauri Shirika la Afya Duniani (WHO) kuangalia uwezekano wa kutumia mifumo ya upatikanaji wa chanjo na dawa muhimu duniani ili kuboresha upatikanaji wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu, hususan katika nchi zinazoendelea.

Mkutano wa COSP19 uliwakutanisha nchi wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu kujadili mafanikio, changamoto na mikakati ya kuimarisha haki, ushiriki na ustawi wa watu wenye ulemavu duniani.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments