Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema kuwa ziara za Rais Samia Suluhu Hassan katika mataifa mbalimbali zina lengo la kuvutia fursa za biashara na uwekezaji, badala ya kutafuta misaada ya kifedha.
Akizungumza leo Juni 11, 2026 bungeni wakati akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/27, Profesa Mkumbo amesema Serikali imeweka msisitizo katika kujenga uchumi unaoongozwa na uwekezaji, biashara na ushiriki mkubwa wa sekta binafsi.
“Mheshimiwa Rais anapofanya ziara za nje anaenda kutafuta washirika wa maendeleo siyo wadhamini, na anatafuta fursa za biashara na uwekezaji, siyo misaada,” amesema Profesa Mkumbo.
Ameongeza kuwa katika kusaka fursa za uwekezaji, Tanzania haitachagua wapi pa kwenda, bali inalenga kufungua milango ya ushirikiano na masoko mbalimbali duniani.
Kauli hiyo imekuja wakati Serikali ikiweka uwekezaji na biashara miongoni mwa sekta muhimu zitakazoongoza mageuzi ya uchumi katika mwaka wa fedha 2026/27. Kwa mujibu wa mpango huo, Serikali inalenga kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kugharamia na kutekeleza miradi ya maendeleo, huku ikiendelea kutafuta washirika wa biashara na uwekezaji kutoka masoko mbalimbali duniani.




