HomeAfyaWRRB yatoa msaada wa vifaa na mahitaji muhimu Hospitali ya Malinyi

WRRB yatoa msaada wa vifaa na mahitaji muhimu Hospitali ya Malinyi

Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala nchini (WRRB) imetoa msaada wa vifaa vya usafi na vyakula kwa Hospitali ya Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa shughuli zake za uwajibikaji kwa jamii.

Msaada huo uliokabidhiwa katika Wodi ya Wazazi ya hospitali hiyo unalenga kuwasaidia wanawake waliojifungua pamoja na kuchangia ustawi wao na kuimarisha huduma za afya kwa jamii.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Asangye Bangu, amesema taasisi hiyo inaamini kuwa mafanikio ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala yanapaswa kwenda sambamba na kuchangia maendeleo ya jamii zinazozunguka maeneo yake ya utekelezaji.

Amesema WRRB inatambua umuhimu wa kushirikiana na jamii na kurejesha sehemu ya mafanikio yanayotokana na utekelezaji wa majukumu yake kwa kusaidia makundi mbalimbali yenye uhitaji.

“WRRB inatambua umuhimu wa kushirikiana na jamii na kurejesha sehemu ya mafanikio yanayotokana na utekelezaji wa majukumu yake. Tunafarijika kuungana na Hospitali ya Wilaya ya Malinyi katika kuwasaidia akina mama waliopo wodini,” amesema Bangu.

Ameeleza kuwa itaendelea kusimamia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala nchini sambamba na kuimarisha ushirikiano na jamii kupitia utekelezaji wa programu mbalimbali za kijamii zinazolenga kuchochea maendeleo na ustawi wa wananchi.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Dk. Julius Nyasongo, ambaye alipokea msaada huo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Wakili Sebastian Waryuba, ameishukuru WRRB kwa msaada huo akisema utakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha ustawi wa akina mama wanaopata huduma katika hospitali hiyo.

“Tunawashukuru WRRB kwa moyo wao wa kujitolea na kuendelea kushirikiana na sekta ya afya. Msaada huu utakuwa na mchango mkubwa kwa akina mama wanaopata huduma katika hospitali yetu,” amesema Dk. Nyasongo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments