HomeHabariJukwaa la NaCoNGO kukutanisha wadau 3,000 Dodoma

Jukwaa la NaCoNGO kukutanisha wadau 3,000 Dodoma

Washiriki zaidi ya 3,000 wanatarajiwa kushiriki Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 2026 litakalofanyika Oktoba 20 hadi 22 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, likiwa na lengo la kujadili mustakabali wa sekta hiyo na kuimarisha mchango wake katika maendeleo ya taifa.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Juni 12,2026, Katibu Mkuu wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Francisca Damian, amesema maandalizi ya jukwaa hilo yanafanyika kwa ushirikiano na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

Amesema kaulimbiu ya mwaka huu ni “Fikra Mpya Kuhusu Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali: Ubunifu, Ubia na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha Kupitia Vyanzo vya Ndani,” ikilenga kuhimiza ubunifu, ushirikiano na kuongeza uwezo wa mashirika hayo kujitegemea kifedha.

Kwa mujibu wa Francisca, jukwaa hilo litawakutanisha viongozi na watendaji wa mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, taasisi za utafiti, vyombo vya habari na wananchi kujadili namna ya kuifanya sekta hiyo kuwa imara, yenye uwajibikaji na mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema mjadala utaweka mkazo katika kupunguza utegemezi wa ufadhili wa nje kwa kuimarisha vyanzo vya ndani vya mapato, kukuza ubia na sekta binafsi, kutumia teknolojia na ubunifu pamoja na kuendeleza mifumo madhubuti ya uwazi na uwajibikaji.

Mbali na mijadala, jukwaa litatoa fursa ya kuonesha mafanikio yaliyofikiwa, changamoto zinazoikabili sekta na fursa mbalimbali za kuimarisha shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali nchini.

Washiriki wanatarajiwa kutoka ndani na nje ya Tanzania, ikiwemo ukanda wa Afrika Mashariki, ambapo maazimio na mapendekezo yatakayopatikana yanatarajiwa kuboresha mazingira ya utendaji wa mashirika hayo na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya wadau.

Francisca amesema kabla ya jukwaa la kitaifa kutafanyika majukwaa ya ngazi ya wilaya mwezi Juni na Julai, pamoja na ya mikoa kati ya Agosti na Septemba 2026, kwa lengo la kukusanya maoni na mapendekezo yatakayowasilishwa katika mkutano mkuu.

Aidha, NaCoNGO imetoa wito kwa mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, vyombo vya habari na wananchi kushiriki kikamilifu katika jukwaa hilo, ikisisitiza kuwa sekta hiyo imeendelea kuwa mshirika muhimu wa Serikali katika elimu, afya, uwezeshaji wa wanawake na vijana pamoja na ustawi wa jamii.

Francisca amehitimisha kwa kueleza kuwa Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 2026 litakuwa fursa ya kutafakari mafanikio yaliyopita, hali ya sasa na mwelekeo wa baadaye wa sekta hiyo, huku NaCoNGO ikiendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha maandalizi yanafanyika kwa weledi na kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments