Dubai, 12 Juni 2026: Airtel Africa Foundation, taasisi ya hisani ya kampuni ya Airtel Africa plc, imezindua ripoti yake ya kwanza ya mwaka, hatua inayohitimisha mwaka wake wa kwanza wa utekelezaji na kuonesha mchango wake kwa mamilioni ya wanafunzi na jamii barani Afrika.
Katika kipindi hicho, Foundation hiyo ilitoa uwekezaji wa dola milioni 6.2 kwa miradi inayotekelezwa kupitia nguzo zake nne za kimkakati ambazo ni Ujumuishi wa Kifedha, Elimu, Uendelevu wa Mazingira na Ujumuishi wa Kidijitali (FEED), ambapo sekta ya elimu ilipata sehemu kubwa zaidi ya fedha hizo.
Mafanikio makubwa ni pamoja na kuunganisha shule 1,028 na huduma ya intaneti kupitia ushirikiano na UNICEF, hatua iliyofanya jumla ya shule zilizounganishwa kufikia 3,296 katika nchi 13, na kuwafikia zaidi ya wanafunzi milioni 2 pamoja na walimu karibu 39,000.
Aidha, majukwaa 64 ya kidijitali yasiyotozwa gharama yamewawezesha zaidi ya wanafunzi milioni 11 kupata maudhui ya elimu bure, jambo lililoongeza upatikanaji wa elimu kwa njia ya mtandao.
Foundation hiyo pia imeboresha miundombinu ya shule za umma kupitia Mpango wa School Adoption, ambapo shule saba zimekamilika kufanyiwa ukarabati mkubwa na 43 zikiwa katika hatua za maboresho, kwa lengo la kuunganisha miundombinu bora na upatikanaji wa elimu ya kidijitali.
Kupitia mpango wa Airtel Africa Tech Fellowship, jumla ya udhamini 257 wa masomo ya chuo kikuu umetolewa katika nchi za Malawi, Nigeria, Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda, hatua inayolenga kukuza elimu ya STEM na kuandaa viongozi wa baadaye katika sekta ya teknolojia barani Afrika.
Zaidi ya vijana na wanawake 30,530 pia wamepatiwa mafunzo ya ujuzi wa kidijitali kupitia programu mbalimbali zinazotekelezwa kwa ushirikiano na serikali na sekta binafsi.
Mwenyekiti wa Airtel Africa Foundation, Segun Ogunsanya, amesema taasisi hiyo ilianzishwa ili kuondoa vikwazo vinavyosababishwa na ukosefu wa fursa sawa, akibainisha kuwa ingawa vipaji vipo kwa wingi, upatikanaji wa elimu, zana za kidijitali na fursa za kiuchumi bado ni changamoto.
Ripoti hiyo pia imeonyesha msisitizo wa taasisi hiyo katika kupima matokeo ya kazi zake na kuleta mabadiliko ya muda mrefu katika jamii.
Katika mwaka ujao, Foundation inapanga kupanua programu zake ikiwemo kuongeza idadi ya shule zitakazonufaika na Mpango wa School Adoption kufikia zaidi ya 80, kuongeza udhamini wa masomo hadi zaidi ya vijana 600, kuunganisha shule nyingine 2,000 na huduma ya intaneti bila malipo, pamoja na kupanua mafunzo ya ujuzi wa kidijitali na ujumuishi wa kifedha kwa jamii zilizo nyuma kimaendeleo.
Ogunsanya aliongeza kuwa taasisi hiyo imejipanga kutoa mafunzo ya ujuzi na mabadiliko endelevu kwa ngazi ya mtu binafsi na kaya, huku ikiunga mkono serikali katika kuharakisha mageuzi ya kiuchumi barani Afrika.




