Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azan Zungu ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuunga mkono jitihada za kuboresha huduma kwa jamii hasa katika sekta ya elimu inayowagusa watu wengi.
Spika Zungu ametoa pongezi hizo aliotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mfano ya Benki ya CRDB (CRDB Bank Secondary Model School) inayojengwa Upanga katika Halmashauri ya Ilala kwa gharama za shilingi bilioni 5.
“Napongeza Benki ya CRDB hasa Mkurugenzi Mtendaji, Dkt. Abdulmajid Nsekela kwa jinsi mnavyojitoa kwa jamii. Leo mnajenga shule hii hapa Ilala ila itawahudumia wanafunzi kutoka kila mahali. Hii inadhihirisha jinsi mnavyotambua na kuthamini elimu kwa watoto wa Kitanzania. Nikuombe mkandarasi, ongeza kasi ujenzi ukamilike mapema,” amesema Spika Zungu.





Akieleza kuhusu mradi huo, Mkurugenzi wetu wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, TullyEsther Mwambapa amesema jengo hilo la shule ya sekondari itakuwa na ghorofa (floors) nne, maabara, ofisi za walimu na vitu vingine muhimu kwa ajili ya kutoa elimu bora kwa wanafunzi.
“Mwanafunzi akishafika shule hatotakiwa kuondoka. Kila kitu kitakuwa ndnai ya jengo hili ambalo litakuwa na lifti. Benki ya CRDB ni mdau mkubwa wa serikali katika kuwahudumia wananchi,” amesema Tully.






Tully amesema itakuwa shule bora na ya kisasa na ameishukuru serikali ya Manispaa ya Ilala kwa kui amini na kushirikiana na Benki ya CRDB katika jitihada za kuboresha maisha ya wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Tanzania nzima kwa ujumla kwani sekondari hiyo itapokea wanafunzi kutoka kila kona ya nchi.
Kuhusu kukamilika kwa ujenzi huo, Mhandisi Anna Mafoka, mkandarasi anayesimamia mradi huo amesema mkataba ulitaka shule hiyo ijengwe kwa miezi 10 na kukamilika Machi mwakani lakini watajitahidi majengo yawe tayari kwa matumizi ifikapo Desemba ili Januari 2027 yaanze kutumika.










