Wito umetolewa kwa makampuni makubwa ya uchimbaji madini nchini kuwekeza katika kuwawezesha wachimbaji wadogo katika nyanja mbalimbali ikiwemo teknolojia za kisasa na usimikaji wa mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi ili kujenga uchumi jumuishi unaotokana na sekta ya madini.
Wito huo umetolewa na serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, alipofanya ziara ya kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi na Sheria nyingine za kazi katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML).
Waziri Sangu ameipongeza menejimenti ya Mgodi huo kwa kuzalisha ajira nyingi kwa Watanzania ambapo GGML imeajiri jumla ya wafanyakazi 2,366 moja kwa moja na 4,629 wameajiriwa kupitia wakandarasi mbalimbali wanatoa huduma katika Mgodi wa GGML.




Sambamba na pongezi hizo, Waziri mwenye dhamana ya masuala ya kazi ameutaka Mgodi huo kuhakikisha kwamba shughuli zake zinakuwa na athari chanya katika uchumi wa jamii zinazowazunguka kwa kutoa fursa za kazi za muda mfupi ikiwemo kuwezesha miradi mbalimbali ya kijamii.
Aidha, Waziri Sangu ameipongeza GGML kwa kuchagua suala la usalama na afya kwa wafanyakazi kuwa tunu yao ya kwanza katika shughuli zao za uchimbaji na uchakataji wa madini jambo ambalo limewafanya kujenga mifumo madhubuti ya kulinda afya na usalama wa wafanyakazi inayozingatia matumizi ya teknolojia za kisasa.
“Ninawapongeza kwa kuweka usalama na afya kama tunu yenu ya kwanza na hii imejidhirisha katika wasilisho lenu mlilofanya hapa ambapo masuala ya usalama na afya yamechukua nafasi ya juu zaidi ya biashara mnayofanya,” ameeleza Waziri Sangu na kuongeza:




“Pongezi hizi inastahili pia Taasisi ya OSHA ambayo imekuwa ikiwaongoza katika kutekeleza hayo kupitia usimamizi mzuri wa Sheria Na.5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 na miongozo mbalimbali chini ya sheria hiyo ambayo wamekuwa wakiitoa kupitia kaguzi zao za mara kwa mara.
”Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Abdallah Komba, amesema OSHA ni miongoni mwa Taasisi zenye msaada mkubwa katika kuwezesha shughuli mbalimbali za kiuchumi kufanyika kwa tija katika Mkoa wa Geita.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema ziara hiyo, inalenga kuona jinsi OSHA inavyoshirikiana na wadau wake kutekeleza Sheria ya Usalama na Afya mahali pa kazi ambayo dhima yake kuu ni kulinda nguvukazi ya Taifa dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi pamoja na kulinda uwekezaji kupitia kuzuia uharibifu wa mali.
Awali, menejimenti ya GGML iliwasilisha taarifa juu ya shughuli zao iliyoainisha jinsi afya na usalama wa wafanyakazi unavyozingatiwa katika shughuli husika. Miongoni mwa masuala yaliyoelezwa katika taarifa hiyo ni pamoja na historia ya mgodi ambapo imeelezwa kuwa madini katika mgodi huo yaligunduliwa mnamo mwaka 1898 na uchimbaji rasmi kuanza mwaka 1999.






