📌Watendaji wajengewa uwezo matumizi ya mfumo wa PD-MIS Ruvuma
Serikali imeendelea kuimarisha huduma kwa watu wenye ulemavu kwa kuwajengea uwezo watendaji wake kutumia mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji na usimamizi wa taarifa unaojulikana kama PD-MIS.
Mafunzo hayo yaliyofanyika mkoani Ruvuma Region yamewahusisha Maafisa TEHAMA na Ustawi wa Jamii kutoka mikoa ya Ruvuma, Mtwara, Lindi na Njombe, yakilenga kuboresha ukusanyaji wa takwimu sahihi kuanzia ngazi ya kaya hadi mkoa.
Kwa mujibu wa Jackob Mwinula kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, mfumo huo utawezesha watu wenye ulemavu kusajiliwa, kupata namba za utambulisho na kufikia huduma muhimu za kijamii kwa urahisi.




Naye Suzana Mayengo amesema mafunzo hayo pia yanawasaidia watendaji kutambua aina mbalimbali za ulemavu na kuhakikisha ushirikishwaji wao katika mipango ya maendeleo.
Kwa upande wake, Antony Nchimbi kutoka e-Government Authority (e-GA) amesema mfumo wa PD-MIS umeunganishwa na mifumo mingine 11 ya serikali ikiwemo elimu, afya na mikopo ili kurahisisha utoaji wa huduma.
Hatua hiyo inatarajiwa kusaidia Serikali kupata takwimu sahihi na kuboresha huduma kwa watu wenye ulemavu, sambamba na kutekeleza Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2006.







