Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umekabidhi rasmi mradi wa matundu 10 ya vyoo wenye thamani ya Shilingi milioni 30 katika Shule ya Msingi Maendeleo iliyopo Kibaha, mkoani Pwani, unaolenga kuboresha miundombinu ya usafi na mazingira ya kujifunzia. Hafla ya makabidhiano ya msaada huo imefanyika leo, Machi 25, 2026.
Akizungumza katika hafla hiyo, mwakilishi wa PSSSF Meneja wa Kanda ya Mashariki Bi. Zaida Mahava ameeleza kuwa msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Mfuko ya kuwekeza na kurejesha kwa jamii (Corporate Social Investment), kupitia kampeni ya #PSSSFKaribunaJamii.




Amebainisha kuwa PSSSF inatambua umuhimu wa afya bora kwa wanafunzi kama msingi wa mafanikio ya kitaaluma, hivyo miundombinu hiyo itasaidia kuimarisha usafi na kuwawezesha wanafunzi kusoma kwa utulivu.
Aidha, msaada huo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu nchini ili kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata elimu katika mazingira salama na yenye hadhi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, ambaye pia ni Afisa Elimu Msingi Wilaya, Bw. Adinari Livamba, ametoa shukrani za dhati kwa Uongozi wa PSSSF kwa uwekezaji huo mkubwa katika sekta ya elimu. Bw. Livamba amebainisha kuwa mradi huo ni wa kipekee na wa mfano wa kuigwa ndani ya Manispaa ya Kibaha.


“Napenda kuushukuru uongozi wa PSSSF kwa moyo huu wa kipekee. Vyoo hivi ni mfano wa kuigwa kwani kwa sasa hakuna vyoo vizuri ndani ya Manispaa ya Kibaha kama hivi tulivyopatiwa na PSSSF leo,” alisema Bw. Livamba. Aliongeza kuwa miundombinu hiyo ni mkombozi kwa wanafunzi na itasaidia kupunguza changamoto za kiafya shuleni hapo.
Hafla hiyo imehitimishwa kwa kauli mbiu ya PSSSF ya “Leo, Kesho, Pamoja,” ikidhihirisha dhamira ya mfuko huo ya kuendelea kuwa mdau muhimu katika maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla nyakati zote.








