Tuesday, May 19, 2026
spot_img
HomeElimuKongamano la AI: Wito watolewa vyuo vikuu kubadili mfumo wa ufundishaji

Kongamano la AI: Wito watolewa vyuo vikuu kubadili mfumo wa ufundishaji

Kongamano la taifa kuhusu akili unde (AI) na msimbo wa picha (QR Code) linaloendelea jijini Arusha limeibua hoja ya kutaka baadhi ya vyuo vya elimu ya juu nchini kuachana na mfumo wa zamani wa ufundishaji na kwenda sambamba na kasi ya ukuaji wa teknolojia na taarifa duniani.

Akizungumza katika kongamano hilo la NAIC Mei 19, 2026, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sayansi na Teknolojia wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Haroun Makandi amesema baadhi ya taasisi tayari zimeanza kuandaa mitaala itakayojumuisha matumizi ya akili unde katika ufundishaji.

Dk. Makandi, aliyemwakilisha Waziri wa Elimu, Adolph Mkenda, amesema baadhi ya vyuo vikuu bado vinaendelea kutumia mbinu za kitamaduni za ufundishaji ambazo haziendani na mahitaji ya dunia ya sasa.

“Utamaduni wa mwalimu kujifungia darasani na kufundisha kama zamani unaonesha wazi kupitwa na wakati. Taasisi zisipobadilika zinaweza kuanguka,” amesema Dk. Makandi.

Ameeleza kuwa mataifa mbalimbali yanaendelea kufanya tafiti kuhusu namna ya kutumia AI kuboresha ufundishaji na ujifunzaji, huku kongamano hilo likitambua umuhimu wa kutumia teknolojia hiyo pamoja na QR Code katika sekta ya elimu.

Akizungumzia nafasi ya lugha ya Kiswahili katika maendeleo ya teknolojia, Dk. Makandi amesema AI inapaswa kutumika kuijenga Kiswahili kama lugha kamili inayoweza kujitegemea bila kutegemea lugha za kigeni.

Amesema Kiswahili ni rasilimali muhimu kwa kuwa kina wazungumzaji zaidi ya milioni 200 ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), jambo linalotoa nafasi kubwa ya kutumia AI katika mazingira ya Kitanzania na Kiafrika.

Kwa upande wake, mdau wa bunifu za teknolojia ya habari na mawasiliano, Faustine Mgimba amesema lengo kuu ni kuhakikisha teknolojia inatumika kuleta mabadiliko chanya kwa kila Mtanzania bila kumuacha mtu nyuma.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments