Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam, amewasili Ikulu ya Dar es Salaam na kupokelewa kwa heshima na mwenyeji wake, Rais Dk Samia Suluhu Hassan.
Mapokezi hayo yaliambatana na gwaride la heshima na mizinga 21 iliyopigwa, ikiwa ni ishara ya saluti kwa kiongozi huyo wa ngazi ya juu wa Singapore.
Ziara hiyo ni ya kihistoria na ya kwanza kufanywa na Rais wa Singapore nchini tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo, mwaka 1980.
Historia nyingine inayoandikwa katika ziara hiyo ni kwamba, inafanyika wakati ambao Tanzania na Singapore zinaadhimisha miaka 45 ya uhusiano wa kidiplomasia.
Rais Shanmugaratnam, anafanya ziara hiyo kwa siku tatu kuanzia Juni 8 hadi 10, mwaka huu. Ziara hiyo, inaendana na mkakati wa Tanzania wa kuimarisha diplomasia ya uchumi, ili kuvutia uwekezaji, teknolojia, masoko na utaalamu.
Katika ziara hiyo, maeneo kadhaa ya ushirikiano yatajadiliwa, ambayo ni biashara na uwekezaji, maendeleo ya bandari na usafirishaji, uchumi wa kidijitali, elimu na mafunzo ya ujuzi, utalii, miundombinu, teknolojia na ubunifu na maendeleo endelevu.
Mapokezi hayo, yamefanyika leo, Jumanne Juni 9, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam.








