Serikali ya Tanzania na Serikali ya Singapore zimefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi baada ya kusaini rasimu ya mikataba na hati tano za makubaliano zitakazolenga kuimarisha biashara, uwekezaji, maendeleo ya rasilimali watu na ushirikiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa ziara ya kihistoria ya Tharman Shanmugaratnam nchini Tanzania, ambapo alifanya mazungumzo ya uwili na Samia Suluhu Hassan jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Rais Samia amesema Tanzania na Singapore zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali zikiwemo biashara, uwekezaji, maendeleo ya vijana na uchumi wa kidijitali.
Amesema pia ameikaribisha Singapore kufungua ubalozi wake nchini Tanzania ili kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya mataifa hayo.
“Nimemweleza dhamira ya Tanzania ya kuwawezesha vijana kupitia elimu ya ujasiriamali, ukuzaji wa ujuzi na ubunifu, huku Serikali ikiendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali wa mwaka 2024–2034,” amesema Rais Samia.
Kwa upande wake, Rais Shanmugaratnam amesema nchi hizo zimekubaliana kushirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo mapambano dhidi ya ugonjwa wa selimundu, uwekezaji katika sekta ya kilimo na kuimarisha biashara kupitia soko huru la Afrika.
Katika hafla hiyo, pande hizo mbili zilisaini rasimu ya mkataba wa kuondoa utozaji kodi mara mbili na kuzuia ukwepaji wa kodi, pamoja na hati za makubaliano kuhusu maendeleo ya ujuzi, mashauriano ya kidiplomasia, biashara ya kaboni na uwezeshaji wa biashara.
Ziara ya Rais Shanmugaratnam imeandika historia mpya kwa kuwa ni ya kwanza kufanywa na Rais wa Singapore nchini Tanzania tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mwaka 1980.
Aidha, ziara hiyo imefanyika wakati Tanzania na Singapore zikiadhimisha miaka 45 ya uhusiano wa kidiplomasia, hatua inayotajwa kuwa sehemu ya mkakati wa Tanzania wa kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa lengo la kuvutia uwekezaji, teknolojia, masoko na utaalamu kutoka mataifa mbalimbali duniani.





